Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Ndugu Daniel Gidfrey Chongolo akizungumza na Wanachama wa CCM pamoja na wananchi wengine kwa ujumla, aliposhiriki katika Mkutano wa Shina Namba 9, Tawi la Kalakala, kwa Balozi Ndugu Salvatory Damian, Kata ya Muze, Jimbo la Kwela Sumbawanga Vijijini, Oktoba 10, 2023, wakati wa ziara yake ya siku nne ya kuimarisha uhai wa chama, kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya 2020-2025, mkoani Rukwa.
Kupitia mkutano huo wa shina, Ndugu Chongolo ameahidi kwenda kuisukuma serikali kuharakisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Muze ambacho kitahudumia wananchi wengine wa maeneo ya karibu pia, na kuhakikisha ujenzi wa barabara inayopita Mlima Lyamba lya Mfipa, hasa kuanzia eneo la Kizungu hadi Muze inayokwenda katika Kata ya Muze Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, yenye urefu wa kilometa 12 unaharakishwa.
Aliwaambia kuwa kipande hicho nacho kinatakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka, kama ambavyo tayari kipande cha kutokea Ntendo hadi Kizungu, chenye urefu wa kilometa 25, kinaendelea kujengwa na mkandarasi yuko eneo la mradi, ili hatimae kero ya usafiri, usafirishaji na uchukuzi wa abiria na mizigo mtawalia, kutoka maeneo hayo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao, inafika mwisho.