Mkurugenzi Msaidizi wa Ufatiliaji wa Haki, Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Beatrice Mpembo, akizungumza na Fullshangwe kando ya semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu kanuni za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi mjini Morogoro.
Amani Manyaga Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Sheria na Katiba akiwasilisha mada kuhusu kanuni za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi mjini Morogoro.
NA JOHN BUKUKU, MOROGORO
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imewatoa hofu wananchi kujitokeza kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu pamoja na ushahidi ambao utatumika Mahakamani kutokana kutungwa kwa sheria ambayo inawalinda katika kuhakikisha wanakuwa Salama.
Akizungumza leo Oktoba 11, 2023 Mkoani Morogoro katika mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu kanuni za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Haki, Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Beatrice Mpembo, amesema kuwa sheria imeweka mkakati wa kumlinda mtoa taarifa pamoja na shahidi ambaye atatumika kufichua taarifa.
Bi. Mpembo amesema kuwa wakati umefika kwa wananchi kutoa taarifa za uhalifu kipindi ambacho zitahitajika kutumika.
“Kama sheria inavyoelekeza wanapaswa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika ili taarifa hizo ziweze kufanyiwa kazi, pia wamewekewa ulinzi wao kama watoa taarifa pamoja na mashahidi ambao watatumika katika kuwakamata wahalifu” amesema Bi. Mpembo.
Amesema kuwa awali kulikuwa na changamoto ya kutokuwa na sheria maalum kwa ajili ya ulinzi wa mashahidi au watoa taarifa na kusababisha asilimia kubwa ya wananchi kuogopa kutoa ushirikiano wa kujihusisha moja kwa moja katika masuala ya ushahidi.
“Wananchi walikuwa wanaogopa kwa sababu walikuwa hawajui watajilinda vipi baada ya kutoa ushahidi wa taarifa za uhalifu kwani wanaotenda uhalifu wanatoka katika jamii” amesema Bi. Mpembo.
Amesema kuwa mashauri mengi yamekuwa yakishindwa Mahakamani kutokana na kukosa watu wa kuwa na utayari wa kutoa ushahidi Mahakamani kwa kuhofia usalama wao.
Amesema kuwa kutokana na changamoto hizo Serikali iliona ni vyema kutunga sheria itakayowalinda watoa taarifa pamoja na mashahidi.