*Rais Mstaafu Kikwete ampongeza Dkt. Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*
*Chalinze imetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020- 2025 kwa mafanikio*
Chalinze – Pwani
Serikali imeahidi kushughulikia changamoto ya umeme iliyopo nchini kwa kasi kubwa ili tatizo hilo liweze kuisha katika kipindi kifupi kuanzia sasa.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 11, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko katika Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo la Chalinze wa kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2020-2025) wilaya ya Chalinze mkoa wa Pwani.
Dkt. Biteko amesema kuwa, katika kipindi cha miezi sita inayokuja ukosefu wa umeme nchini utaisha baada ya Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kumaliza tatizo hilo nchini. Amesema Watendaji wanafanya kazi ili watanzania wapate umeme wa kutosha.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza TANESCO kupeleka umeme katika shule ya Sekondari ya Moreto ili shule hiyo iunganishwe na umeme mapema. Aidha amechangia kompyuta 10 kwenye shule hiyo maalum kwa matumizi ya TEHAMA kuwasaidia wanafunzi.
Kuhusu Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Dkt. Biteko ametumia nafasi hiyo kupongeza juhudi zinazofanywa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo ujenzi wa madarasa, zahanati na miundombinu muhimu na pia kufanya vizuri katika makusanyo ya mwaka ambapo wilaya hiyo imekusanya shilingi bilioni 15.
Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa msukumo mkubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu na fedha hizo zinaelekezwa katika miradi mbalimbali ili kukuza uchumi wa nchi.
Vile vile, Mhe. Dkt. Kikwete amempongeza Mhe. Dkt. Biteko kwa kuteuliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati hapa nchini na kumsisitiza awe msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali na kufanya kazi kwa bidii.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa mkoa wa Pwani unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule, madaraja, vituo vya afya ili mkoa huo ukue kiuchumi na hatimaye kuboresha maisha ya wananchi wake.
Aidha, Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema, katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, halmashauri ya wilaya ya Chalinze imefanikiwa kutekeleza kwa kiwango kikubwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/25.
“Wananchi wamewezeshwa kiuchumi, hali ya uzalishaji katika Kilimo, uvuvi, umwagiliaji, viwanda na biashara imeongezeka, miundombinu ya shule, zahanati, vituo vya afya na hospitali ya wilaya imekamilika kwa asilimia kubwa na kwenye baadhi ya vijiji na kata ujenzi unaendelea,” amesema Mhe. Ridhiwani.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okash amesema, katika uongozi wa miaka wa Rais Samia wameshuhudia mabadiliko makubwa kimaendeleo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze. Amesema Mbunge anaonesha ushirikiano
Wilaya ya Bagamoyo ni miongoni mwa wilaya Saba zinazounda mkoa wa Pwani. Wilaya hiyo ina halmashauri Kuu mbili ambazo ni Halmashauri ya wilaya ya Chalinze na Halmashauri ya Bagamoyo.
Mkutano huo umehudhuriwa na Viongozi Mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wanachama zaidi ya 1000 walioshiriki katika uwasilishwaji wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi CCM 2020/25