Afisa Elimu Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Martha Ngalowera akitoa elimu ya Muungano na Mazingira kwa wananchi waliotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa inayofanyika Babati, mkoani Manyara kuanzia Oktoba 8 hadi Oktoba 14 ambapo inakwenda sambamba na uzimwaji wa Mwenge wa Uhuru 2023.
Mhandisi Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Onespholy Kamukuru akitoa elimu ya Muungano na Mazingira kwa wanafunzi waliotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa inayofanyika Babati, Mkoani Manyara kuanzia Oktoba 8 hadi Oktoba 14, 2023 ambapo inakwenda sambamba na uzimwaji wa Mwenge wa Uhuru 2023.
Mhandisi Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Onespholy Kamukuru akiongea na Waandishi wa Habari juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa inayofanyika Babati, mkoani Manyara kuanzia Oktoba 8 hadi Oktoba 14, 2023 ambapo inakwenda sambamba na uzimwaji wa Mwenge wa Uhuru 2023.
Wanafunzi wakisoma vitabu vya historia ya Muungano katika Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais kwenye maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa inayofanyika Babati, mkoani Manyara kuanzia Oktoba 8 hadi Oktoba 14 ambapo inakwenda sambamba na uzimwaji wa Mwenge wa Uhuru 2023.
Baadhi ya wananchi wakiwa Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa inayofanyika Babati, mkoani Manyara kuanzia Oktoba 8 hadi Oktoba 14 ambapo inakwenda sambamba na uzimwaji wa Mwenge wa Uhuru 2023.
………
Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika Babati mkoani Manyara.
Maonesho hayo yanayokwenda sambamba na uzimwaji wa Mwenge wa Uhuru 2023 yameanza Oktoba 8 na kutarajiwa kumalizika Oktoba 14, 2023.
Akitoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda hilo Afisa Elimu Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Martha Ngalowera amesema vijana wanaweza kujipatia kipato kwa kuangalia fursa mbalimbali za utunzaji wa mazingira zinazopatikana katika eneo analoishi.
Bi. Martha amesema mazingira yanatoa fursa nyingi kwa vijana kama vile upandaji wa miti wa matunda unavuna matunda na kujipatia fedha lakini hata miti yenyewe ni biashara kubwa.
“Utunzaji wa taka unaweza ukazalisha mbolea ambapo inatumika na watu wengi katika mashamba na watunza bustani hiyo yote ni biashara ambayo kijana anaweza akafanya kujipatia kipato wakati huohuo anatunza mazingira.
“Kwa mfano unapokusanya chupa, kuna viwanda ambavyo hutumia tena hizo chupa kwa matumizi mbalimbali, hapo unaona kwamba unaweka mazingira safi na pia kupata fedha kwa biashara hiyo,” amesema Bi. Martha.
Kwa upande wake Mhandisi Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Onespholy Kamukuru amesema lengo la uwepo wao katika ‘Wiki ya Vijana’ ni kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
“Tumeandaa mada ambayo inaelezea nafasi ya vijana katika uhifadhi wa mazingira, kikubwa tunaangalia shughuli ambazo vijana wanazifanya kwaajili ya kuongeza kipato ikiwemo kuwa na shughuli za uhifadhi kama vile ufugaji wa nyuki, utunzaji wa taka ambapo vijana wanaweza wakaungana na kuwa kikundi na kujipatia kipato.
“Aidha tunatoa historia ya Muungano ambapo wanafunzi wamekuwa wakinufaika wakubwa wa elimu hii ambayo naamini kuna baadhi ya vitu wanajifunza shuleni na hapa tunawaongezea maarifa mengine hata yale ambayo hawakuyapata huko.”
Mhandisi Kamukuru ameongeza katika uhifadhi wa mazingira kumekuwa na fursa nyingi kwa vijana kwa kuandika maandiko na kupata fedha ambapo wamekuwa wakisaidiwa kupata wafadhili kutokana na maandiko yao ya miradi hasa yanayoendana na uhifadhi wa mazingira.
Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2023 yanafanyika Babati mkoani Manyara ambapo ujumbe ni “Vijana na ujuzi rafiki wa mazingira kwa maendeleo endelevu.”
Aidha, ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu 2023 unaohusu Mabadiliko ya Tabianchi Hifadhi Mazingira sambamba na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji “Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai kwa Uchumi wa Taifa.”