Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Wizara ya Kilimo hapa nchini kufanikisha lengo lililowekwa na Wizara hiyo la kuacha kuuza Korosho ghafi nje ya nchi ifikapo mwaka 2026.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuendelea kuuza korosho isiyochakatwa (ghafi) kunasababisha kupunguza ajira za watanzania, kupunguza mapato ya fedha za kigeni pamoja na upatikanaji wa bidhaa zitokanazo na zao la korosho kama vile maziwa, mvinyo, juisi na mafuta.
Aidha Makamu wa Rais amesema ni muhimu mkutano huo ukajadili na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuimarisha huduma za ugani na utoaji pembejeo kwa wakati ili kuongeza uzalishaji wa zao la Korosho.
Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa mkutano huo kujadili namna bora ya kuwa na mkakati wa kufikia masoko ya zao la korosho kwa usawa. Amesema kumekuwa na ulaghai kati ya wanunuzi,wasafirishaji na madalali jambo linalothibitishwa na idadi ndogo ya wanunuzi kwenye minada ambao wana ufahamu wa kutosha kuhusu bei za soko huku wakulima wa korosho wakiwa na taarifa ndogo za soko.
Ameongeza kwamba kutokana na hali hiyo, wakulima wa zao la korosho wamekabiliwa na bei isiyo ya haki. Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji kuwekeza katika sekta ya zao la korosho kutokana na taifa kuwa na ardhi ya kutosha ya kilimo na hali nzuri ya hewa.
Ameongeza kwamba kipindi cha mavuno ya korosho nchini Tanzania (Septemba-Desemba) ni msimu wa kutokuwepo kwa wazalishaji wengine wakuu kama vile India, Vietnam na Afrika Magharibi hivyo kutoa fursa kubwa ya soko la zao hilo.
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa nchi za Afrika kujitahidi kupunguza bei ya mlaji wa korosho ili kukuza ongezeko la matumizi ya korosho na bidhaa zitokanazo na zao hilo kitaifa na kikanda.
Amesema kwa kuzingatia uwezo mkubwa wa soko wa Afrika wa takriban watu bilioni 1.4 chini ya ukanda huru wa biashara barani Afrika (AfCFTA). Aidha amezisihi nchi zinazolima korosho barani Afrika kuangalia na kukomesha vitendo viovu katika biashara hiyo kama vile upangaji usio sawa wa madaraja ya korosho na usambazaji wa viuatilifu visivyofaa.Mkutano huo wa siku tatu (Tarehe 11-13 Oktoba 2023) unashirikisha Zaidi ya wadau 500 kutoka nchi 33 zinazozalisha na kula korosho.
Pamoja na mambo mengine lengo la Mkutano huo ni kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko katika mnyororo wa thamani wa zao la korosho.