Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam (Tarehe 11 Oktoba 2023)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde wakati alipowasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kufungua Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho. (Tarehe 11 Oktoba 2023)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kuhusu maendeleo ya zao la korosho kutoka kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania Francis Alfred wakati akitembelea mabanda ya maonesho yaliyopo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam unapofanyika Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho. (Tarehe 11 Oktoba 2023)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wauzaji wa zao la korosho kuhusu umuhimu wa kuzingatia soko la ndani ya nchi na Afrika wakati akitembelea mabanda ya maonesho yaliyopo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam unakofanyika Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho. (Tarehe 11 Oktoba 2023)
Viongozi na wadau mbalimbali wa zao la korosho wakisikiliza hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam (Tarehe 11 Oktoba 2023).
…………………..
Na Sophia Kingimali
Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango amewataka wawekezaji kuja kuwekeza nchini katika zao la Korosho kwani limekua ni zao lenye tija na faida kubwa kwa nchi huku nchi ikitenga maeneo kwa ajili ya uzalishaji wa zao hilo ambapo kuna maeneo yana hali ya hewa nzuri inayofaa kwa ajili ya uzalishaji wa zao hilo.
Aidha Dkt Mpango ameainisha maeneo matatu yatakayohakikisha zao la Korosho linaleta tija kwa taifa na wakulima kwa ujumla ambapo ameyataja maeneo hayo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa masoko ya uhakika, kuimarisha tafiti za zao hilo na kutafuta wawekezaji.
Kauli hiyo ameitoa leo Oktoba 11, 2023 jijini Dar es Salaam leo, wakati akifungua mkutano wa kwanza wa Kimataifa wa zao la Korosho ambao imebebwa na kauli mbiu isemayo ‘Wekeza kwenye Korosho kwa maendeleo endelevu’.
Wadau wanajadili jinsi ya kukuza zao la korosho kwani lina faida nyingi katika mwili wa binanadamu na linachangia kukuza uchumi.
“Wizara ya kilimo hakikisheni mnaimarisha tafiti za zao la Korosho ili kuongeza uzalishaji utakaokidhi masoko na wadau hakikisheni mnatafuta changamoto na kuumizwa kichwa juu ya upatikanaji wa masoko ya uhakika ya zao hilo,” amesema.
Aidha amewata TARI kuhakikisha wanazalisha mbengu bora za zao hilo ili kuendelea kuleta tija kwa wakulima .Aidha Dk Mpango, amesema thamani ya soko la Korosho duniani inakadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 10.5 ifikapo mwaka 2031 kutoka Dola Bilioni 7 mwaka jana, hivyo mkutano huo umekuja kwa wakati ili kuzisaidia nchi zinazozalisha zao hili kuweka mikakati madhubuti ya kunufaika nalo.
Hata hivyo, amesema licha ya jitihada zilizofanywa na nchi mbalimbali ikiwemo Tanzani, bado changamoto ya kuongeza thamani ya zao la Korosho ipo kwa kuwa asilimia 90 ya Korosho inayozalishwa inauzwa nje ikiwa ghafi hali inayoshusha bei lakini pia bidhaa zingine zinazotokana na Korosho kama siagi, mvinyo, juisi, maziwa zinakwenda kwenye nchi zingine na si nchi wazalishaji.
Ameitaja changamoto nyingine kuwa huduma za ugani, pembejeo na teknolojia ambazo ni muhimu katika kuongeza tija ya uzalishaji kwa kuwa wakulima wanahitaji kusaidiwa ili kukabiliana na wadudu waharibifu na magonjwa ya mikorosho.
Dk. Mpango amesema kuna changamoto ya soko inayofanya uuzaji wa zao hilo kwa ufanisi kuwa mgumu kutokana na kuwepo kwa ulaghai kati ya wanunuzi, wasafirishaji na madalali jambo linalowanyonya wakulima kwenye suala la bei, hivyo wadau wa mkutano huo wanapaswa kujadili na kuja na mikakati ya namna nchi wazalishaji zinavyoweza kuondokana na changamoto hizo.
Pia amezitaka nchi za Afrika kupambana kutatufuta changamoto ya zao la Korosho kwa kuondoa utitiri wa kodi.
Hata hivyo Dk.Mpango aliwataka wawekezaji kijitokeza kuwekeza nchini kwani hali ya hewa na ardhi ni nzuri kwa uzalishaji wa zao la Korosho.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, David Silinde amesema lengo la mkutano huo ni kutimiza azma ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuongeza tija kwenye zao la Korosho na kutangaza fursa za uwekezaji ili kufikia malengo ya mwaka 2025 ya kuongeza uuzwaji wa zao hilo nje ya nchi likiwa limebanguliwa.
Amesema mkutano utawapa nafasi ya kujifunza Kwa nchi nyingine jinsi walivyoendelea katika uzalishaji na uongezaji thamani wa zao hilo.
” Mwaka jana uzalishaji nchini ulikuwa Tani 186,000 na mwaka huu tunatarajia kuzalisha Tani 300,000 kutokana na hali nzuri ya hewa tunatarajia ndani ya miaka miwili ijayo kufikia Tani 700,000 huku malengo ya mwaka 2030 ikiwa Tani milioni moja,”amesema.
Amesema ili kufikia malengo hayo inatakwa kuwa na wawekezaji wa kutosha na kuongeza thamani ya mazao kwa sababu nchi ilikuwa ikizalisha Korosho ghafi na asilimia 90 ya Korosho zote zimekuwa zikienda nchi ya India na Vietinam ikiwa gafi.
Silinde amesema baada ya kufanya tafiti wamejiridhisha kuwa ukiuza Korosho ghafi unauza asilimia 50 ya bei halisi hivyo matarajio ya serikali ni kukuza Korosho iliyoongezewa thamani.
Amesema ili kufikia malengo hayo serikali inaongeza wigo wa mikoa inayozalisha Korosho kutoka mikoa mitano ya awali hadi 18 ambapo utafiti umebaini kuwa ardhi ya mikoa hiyo ni nzuri kwa uzalishaji wa korosho.
Amesema malengo ya serikali ni mauzo ya mazao nje kufikia asilimia 10 mwaka 2030 kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.2 hadi Bilioni 5.
Naye Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara, Exaud Kigahe amesema Wizara hiyo itavutia wawekezaji Kwa kuhakikisha asilimia 90 ya zao hilo linauzwa likiwa limebanguliwa.
Amesema asilimia 65 ya watanzania wamejiajiri katika sekta ya kilimo sasa mazao yanapaswa kuongezewa thamani ili kuwa na tija kwa wakulima na nchi.
“Serikali inapaswa kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima wa Korosho huku sekta binafsi zikipewa kipaumbele”amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya kudunu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile amesema tangu serikali ya awamu ya sita iingie madarakani, sekta ya kilimo imekuwa na Maendeleo makubwa.
Amesema zao la Korosho ni la kibiashara na limekuwa likichangia katika pato la taifa hivyo ni bora likaendelea kuwekea mikakati thabiti ya kuendelea kuliimarisha.
“Kamati ya Bunge tunaiomba serikali kuingiza programu ya BBT kwenye uzalishaji wa zao la Korosho ili kuwezwsha kuwepo na mashamba makubwa ya Korosho yenye tija,”amesema
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile amemshukuru Rais Dk.Samia kwa kazi kubwa anayofanya ya kuhudumia wananchi hasa wakulima wa Korosho kwa kuweka juhudi mbalimbali katika sekta kilimo ikiwemo kuongezeka mara dufu kwa bajeti ya wizara ya hiyo.
Amesema Bodi ya Korosho inaunga mkono mkakati wa kuwapa pembejeo wakulima na hivyo ameahidi kufuatilia ubora wa zao hilo na kuhakikisha linahifadhiwa katika magahala.
Aidha bodi itaendelea kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa ajili ya kuleta tija hivyo mkutano huu ni muhimu kwa wadau wa Korosho kujadili mustakabali wa zao hilo.
Mkutano huo unaofanyika kwa siku 3 jijini Dar es salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere JNICC umekutanisha nchi 33 ambapo washiriki zaidi ya 640 wameshiriki.