Neema Haule mkuu mashataka mkoa wa Mororgoro akifungua mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu kanuni za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi yanayofanyika kwa siku mbili kwenye hoteli ya Flomi mkoani Morogoro ambapo mafunzo hayo yameandaliwa na wizara ya sheria na katiba Leo Oktoba 10,2023, kulia ni Barton Mwasomola Mkurugenzi msaidizi idara ya Katiba wizara ya sheria na katiba na kushoto ni Beatrice Mpembo Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya ufuatiliaji haki Wizara ya Sheria na Katiba.
Barton Mwasomola Mkurugenzi msaidizi idara ya Katiba wizara ya sheria na katiba akimkaribisha Neema Haule mkuu mashataka mkoa wa Mororgoro ili kufungua mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwenye hoteli ya Flomi mjini Morogoro kwa siku mbili. 
Amani Manyaga mwasilishaji wa mada ya ulinzi wa watoa taarifa na mashahidi akiwasilisha mada hiyo kwa washiriki wa semina hiyo inayofanyika kwenye hoteli ya Flomi mjini Morogoro.
Josiah Mathama Mratibu Msaidizi programs ya BSAAT (Programu Endelevu ya Kupambana na Rushwa nchini Ofisi ya Rais IKULU akifafanua jambo katika semina hiyo.
Wakili wa Serikali Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria kulia pamoja na maofisa wengine wa wizara hiyo wakiwa tayari kwa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari.
…………………………
JOHN BUKUKU, MOROGORO
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kutumia kalamu katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa za uhalifu pamoja na matendo yote yanayofanywa kinyume cha sheria, kwani taarifa hizo zitakuwa na siri bila kuwataja watoa taarifa na mashahidi.
Akizungumza leo Oktoba 10, 2023 Mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu kanuni za ulinzi kwa watoa taarifa na mashahidi, Mkuu Mashataka Mkoa wa Mororgoro Bi. Neema Haule, amesema kuwa mashahidi wanapaswa kufika Mahakamani bila hofu kwani zipo kanuni ambazo zinawalinda katika changamoto zote kwa usalama wao.
Bi. Haule amesema kuwa kanuni zimebainisha wale ambao watatoa taarifa zitasaidia kuokoa mali za umma, kupatikana kwa wahalifu na kulinda mazingira pamoja na maisha ya binadamu kutokana na uharibifu ambao umepangwa kufanyika, huku akieleza kuwa wamewekewa utaratibu wa kupatiwa motisha.
“Naomba kupitia taalamu yenu ya habari tuendelee kutoa elimu ya kisheria kwa umma kuhusu masuala ya kisheria ili wananchi wawe na uwelewa mkubwa pamoja na kujua umuhimu wa kufichua wahalifu wa makosa mbalimbali yanayotendeka katika jamii yetu” amesema Bi. Haule.
Amesema kuwa utoaji wa taarifa za uhalifu itasaidia kupunguza matukio ya kuvunja sheria au kuisha kabisa katika jamii.
Mkurugenzi Msaidizi idara ya Katiba Wizara ya Sheria na Katiba Bw. Barton Mwasomola amewataka waandishi wa habari kutoa ushirikiano katika kuhabarisha umma katika kuitangaza hiyo sheria na kanuni zake.
Bw. Mwasomola amesema kuwa sheria hiyo imelenga kufichua uhalifu hasa katika masuala ya rushwa pamoja na ukiukaji wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa umma.
“Mkijifunza mtapata uwelewa na nyinyi kwenda kuhabarisha umma ili wananchi wawe huru kutoa taarifa ya kufichua wahalifu” amesema Bw. Mwasomola.