Mwenyekiti wa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo Bw. Vicent Kasambala (kushoto) akimkabidhi Dekano wa Dekania ya Kilimahewa Padre Tito Rwegoshora (katikati) Chakula zaidi ya tani tatu ikiwemo mafuta ya kupikia, Mchele, Sukari, Unga, Maharage, Chumvi Kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji Katika Wilaya ya Mkuranga, Kibiti, Rufiji na Mafia baada ya kumalizika kwa Misa ya Kuadhimisha Somo wa Mtakatifu Vincent wa Paulo iliyofanyika katika Parokia ya Kilimahewa Oktoba 8, 2023 Mkoani Pwani.
Baadhi ya matoleo kutoka Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji katika Dekania ya Kilimahewa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Dekano wa Dekania ya Kilimahewa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Padre Tito Rwegoshora akibariki matoleo kutoka Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji katika Dekania hiyo.
Wanachama wa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo wakipeleka matoleo katika Misa ya Kuadhimisha Somo wa Mtakatifu Vincent wa Paulo iliyofanyika katika Parokia ya Kilimahewa Oktoba 8,2023.
Kamati Tendaji ya Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo wakiwa katika picha ya pamoja na Dekano wa Dekania ya Kilimahewa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Padre Tito Rwegoshora baada Misa ya Kuadhimisha Somo wa Mtakatifu Vincent wa Paulo iliyofanyika katika Parokia ya Kilimahewa Oktoba 8,2023.
NA NOEL RUKANUGA, PWANI
Familia nyingi za Wakazi wanaoishi katika Vijiji mbalimbali Mkoani Pwani wanakabiliwa na Uhaba wa Chakula kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa Elimu ya Kilimo licha ya kuwa na Mashamba ambayo yangeweza kuwasaidia kupata Chakula cha kutosha.
Akizungumzia Oktoba 8, 2023 Mkoani Pwani wakati akipokea zaidi ya tani tatu za Chakula ikiwemo Mchele, Unga, Mafuta, Sukari na Chumvi kutoka Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo Jimbo Kuu la Dar es salaam ili kusaidia watu wenye uhitaji katika Wilaya ya Mkuranga, Kibiti, Rufiji na Mafia, Padre wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam Padre Tito Rwegoshora, amesema kuwa maeneo mengi ya Mkoa wa Pwani kuna changamoto ya ukosefu wa chakula.
Padre Rwegoshora amesema kuwa baadhi ya kaya wanapata chakula mlo mmoja kwa siku jambo ambalo limekuwa tatizo kubwa.
“Kati ya matizo yanayowasumbua watu uku ni ukosefu wa chakula cha kutosha , baadhi ya watu wanaudumavu wa kimo au akili kutokana hawapati chakula cha kutosha” amesema Padre
Rwegoshora.
Padre Rwegoshora amesema pia kuna tatizo la ukosefu huduma muhimu ya Afya kutokana na wengi kutokuwa na Bima za Afya, hivyo kushindwa gharama jambo ambalo linawafanya wengi kuamini zaidi waganga wa kienyeji na kuhusisha na magonjwa na ushirikina.
“Inawezekana wanakwenda kwa waganga ya kienyeji kupata majibu ya matatizo ya afya zao, wengi wanasadiki katika ushirikina, wanadanganyika kirahisi” amesema Padre
Rwegoshora.
Amesema kuwa bado mwamko wa kutafuta elimu upo chini hasa katika kupambana na maadui watatu, hivyo jitihada zinaitaji ili kuhakikisha tunafikia malengo tarajiwa.
Padre Rwegoshora jamii ya kada mbalimbali zinapaswa kuwekeza nguvu katika kueneza imani ya kweli ili kuwakomboa baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Pwani.
“Juhudi zinaitaji ili kuwaondoa katika kifungo cha mawazo na tabia ya ushirikina pamoja na mazingira ambayo yanawakabili” amesema Padre.
Amesema kuwa huduma ya elimu itasaidia katika kuwapatia maarifa pamoja na ujuzi ili kuondoka na umaskini.
Padre Rwegoshora ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza katika kutoa msaada wa vitu mbalimbali ili kuwasaidia wahitaji.
“Tujitokeze kwa ajili ya kufanya matendo ya huruma kwa kutoa mavazi, chakula, bima ya afya pamoja na vitu vingine vitakavyowasaidia kupata mahitaji ya muhimu” amesema Padre Rwegoshora.
Mwenyekiti wa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo Bw. Vicent Kasambala, amesema kuwa pamoja na utume wao kuwa wakusaidia wahitaji kila siku katika Parokia mbalimbali, kila mwaka wamejiwekea utaratibu wa kusaidia kundi kubwa la wahitaji kwa namna tofauti ikiwa na lengo la kuwafariji watu wenye shida.
Bw. Kasambala amesema kuwa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo linafanya kazi la kusaidia watu maskini, wagonjwa pamoja na wafungwa.
“Katika familia zetu kuna watu wanakosa chakula kutoka na sababu mbalimbali ikiwemo uwezo wa kipato, wengine wazee, yatima hivyo wanashindwa kupata chakula kwa wakati” amesema Bw. Kasambala.
Amefafanua kuwa mipango yao ni kuhakikisha wanaendelea kuonesha upendo kwa watu wote hasa wahitaji ambao wapo katika maeneo mbalimbali nchini.
Mtunza hazina wa Shirika hilo Esther Mwita amesema kuwa watu wenye uhitaji ni wengi hivyo amewaomba watu mbalimbali kuendelea kuungana na Shirika hilo kuonyesha upendo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Dekania ya Kilimahewa, Agribeti Mkwela amelishukuru Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo kwa kutoa msaada wa chakula huku akitoa wito kwa watu mbalimbali kutoa msaada kutokana uhitaji bado ni mkubwa.
Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo kwa mwaka huu imeadhimisha somo katika Parokia ya Kilimahewa Mkoani Pwani pamoja na kutoa matoleo zaidi ya tani tatu za chakula kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji.
Pia linatarajia kutoa msaada wa Chakula katika vituo mbalimbali vya Kanisa vilivyopo Jimbo Kuu la Dar es Salaam pamoja na hospitali ya Taifa Muhimbili.