Na. WAF – Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Molel amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza zaidi ya Trilion 6.7 katika sekta ya afya ili kuhakikisha anamaliza Rufaa za Wagonjwa wa nje ya nchi.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Oktoba 8, 2023 wakati akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika mbio za Saifee (SAIFEE MARATHON) zilizoandaliwa na Hospitali ya Saifee katika viwanja vya Green Park Masaki Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwezesha upasuaji wa Saratani ya Matiti kwa wanawake nchini.
Dkt. Mollel amesema kuwa ili kufikia azma hiyo Dkt. Samia ameboresha miundombinu katika sekta ya afya ikiwemo teknolojia katika sehemu ya kutolea Huduma, Upatikanaji wa dawa, pamoja na kusomesha wataalamu wa afya chini ya Programu ya Samia Scholarship.
“Ili kufikia azma ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan lazima tushirikiane na sekta binafsi kwa lengo la kuhakikisha Rufaa za wagonjwa wa Nje zinaisha na kuvutia nchi zanje kufata Huduma za afya nchini kwetu”. Amesema Dkt. Mollel.
Hata hivyo ameongeza kuwa nafasi ya Sekta binafsi nchini katika kufikia azma hiyo ni kubwa sana ambapo malengo ni kumaliza rufaa za wagonjwa wa nje pamoja na kufikia Utalii tiba.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamisi amesema kwa upande wa Zanzibari wameanza kushirikiana na Sekta binafsi na Hospitali ya Saifee inasimamia kuhakikisha Huduma za afya Zanzibar zinapatikana kwa ufasaha.
“Sisi kama Serikali tutahakikisha tunasimamia ubora wa Huduma kwa wananchi kwa kushirikiana na Sekta binafs nchini”. Ameeleza Mhe. Khamis.