Na Mwandishi wetu, Kiteto
MWENGE wa uhuru umeanza mbio zake Mkoani Manyara, ukitokea Mkoa wa Dodoma, ambapo unatarajiwa kukimbizwa kilomita 1,116 kwenye miradi 58 ya thamani ya Sh13.2 bilioni katika Halmashauri saba za Wilaya.
Kilele cha mbio za mwenge wa uhuru kitaifa itafanyika Oktoba 18 mwaka 2023 mjini Babati na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga akizungumza wakati akipokea mwenge wa uhuru kwa mkuu wa mkoa wa Dodoma, Rose Senyamule, amesema wamejipanga ipasavyo kuukimbiza mwenge hadi siku ya kilele Oktoba 14 mjini Babati.
Sendiga amesema ukiwa Manyara, mwenge wa uhuru utazindua, kuona, kukagua, kutembelea na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi huo mbalimbali katika wilaya za Kiteto, Simanjiro, Mbulu, Hanang na Babati.
Amesema katika fedha hizo Sh13.2 bilioni za miradi ya maendeleo, michango ya wananchi ni Sh837 milioni na wadau wa maendeleo Sh500 milioni.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema RC Sendiga.
Amekiri kuupokea mwenge wa uhuru ukiwa unang’ara na kumeremeta, ukiwa na wakimbiza mwenge wa kitaifa na maofisa mbalimbali na ameahidi atawatunza.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka 2023, Abdalah Shaibu Kaim amewapongeza viongozi wa Manyara kwa namna walivyojipanga kwenye mapokezi ya mwenge huo.
“Tunakupongeza RC Manyara mtu bingwa kabisa kwa mapokea haya kweli mmedhihisha kuwa mmejipanga kwenye Oktoba ya kibabe,” amesema Kaim.
Mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa kutoka mkoa wa Manyara, Emmanuel Hondi amewakaribisha viongozi na wananchi wa Dodoma kwenye kilele cha mbio za mwenge wa uhuru mjini Babati.