……………………
Waziri wa Maliasili na Utalii na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesema mashirikiano baina ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania na Oman yatanufaisha pande zote mbili katika uhufadhi wa malikale.
Mhe. Kairuki ameyasema hayo tarehe 7 Oktoba 2023 katika hafla fupi ya kufunga kikao kazi cha kujadili mpangokazi wa utekelezaji wa Mkataba wa Mashirikiano baina ya Makumbusho ya Tanzania na Oman.
Amesema anaamini kuwa utekelezaji wa makubaliano ya mashirikiano utaleta tija kwa makumbusho zote mbili katika maeneo ya uhifadhi, utafiti na kujenga uwezo wa wataalam kuhifadhi mikusanyo kwenye mifumo ya kidigitali itakayowezesha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi zaidi.
” Ni matumaini yangu kuwa mashirikiano haya yatakuwa na tija kwa makumbusho zote mbili na kuchochea maendeleo ya sekta ya malikale” Amesema Mhe. Waziri
Amesema mashirikiano hayo ni mwanzo mzuri wa kukua kwa diplomasia na mashirikiano ya kihistoria baina ya Tanzania na Oman.
Aidha, Mhe. Waziri amesema Oman wamekubali kuboresha onesho la historia na kujenga jengo la ghorofa mbili katika kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Makumbusho ya Oman, Mhe. Jamal Al-Moosawi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali mashirikiano ya Makumbusho ya Taifa ya Tanzania na Oman katika maeneo ya uhifadhi, utafiti na kujenga uwezo wa watendaji wa makumbusho hizo.