Ongezeko la awamu za usambazaji wa dawa kutoka nne kwa mwaka hadi sita umetajwa kusaidia kuondoa uhaba wa dawa katika maeneo ya huduma na kuondoa upelekaji wa dawa zilizokaribia kuisha muda katika vituo vya afya.
Kuongezwa kwa awamu za usambazaji dawa unaofanywa na Bohari ya Dawa (MSD) hivi sasa ulilenga kuondoa malalamiko ya ucheleweshaji wa oda uliokuwa ukifanya baadhi ya vituo kuwa na malalamiko ya kukosa dawa.
Hayo yalielezwa na Mfamasia mkuu mkoa wa Lindi, Richard Nshekela wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya jitihada zinazofanywa na MSD katika usambazaji wa vifaa tiba na vifaa.
Alisema tofauti na zamani ambapo walikuwa wakitumia muda mrefu kupata oda walizoagiza lakini sasa oda hizo zinafika kwa wakati na kuhudumia wananchi kama ilivyokisudiwa.
Alisema usambazaji wa dawa kila baada ya miezi miwili unaofanywa umesaidia kwani kituo kinapowasilisha mahitaji halisi kwa wakati na kupata kinakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi juu ya bidhaa zake.
“Kuna muda tulipokuwa tukicheleweshewa huduma kituo kilikuwa kinapokea hadi oda mbili ndani ya mwezi mmoja na kufanya bidhaa kuwa nyingi tofauti na mahitaji na huwezi kurudisha inabidi uzitunze,” alisema Nshekela.
Alisema tofauti na sasa oda huchakatwa ndani ya siku 20 kabla ya dawa kufanyiwa usambazaji moja kwa moja katika vituo jambo ambalo limefanya upatikanaji wa dawa vituoni kuwa asilimia 94.
Suala hilo liliungwa mkono na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk Kheri Kyaga aliposema upatikanaji wa bidhaa umeboreshwa huku akisema eneol hilo lilikuwa kati ya yale yaliyokuwa na shida.
Hiyo ni kutokana na kile alichoeleza kuwa oda zilizokuwa zikipelekwa na ikiwa zinapaswa kuagizwa basi ilihitajika hadi miezi minne tofauti na sasa wanapokuwa na akiba.
“Hili lilifanya kusambaza dawa ambazo zinakaribia kuisha muda mzigo unakuja ukiwa umebaki kuwa na muda wa matumizi ndani ya miezi sita au mwaka mmoja lakini sasa hili halipo,” alisema Dk Kheri
Alisema kuongezeka kwa uwazi ndani ya bohari ya dawa pia moja ya kitu kikubwa ambacho kimefanyika.
“Uwazi umeongezeka kwa mifumo ya taarifa kuonekana inayowezesha watu kujua bidhaa zilizopo, fedha zilizopo, oda jinsi zinavyofanyiwa kazi, pia uwezo wa kusambaza dawa umeongezeka kutoka miezi mitatu kwa kituo hadi miezi miwili ni hatua kubwa,” alisema Dk Kheri.
Kufanyika kwa maboresho haya kumefanya thamani ya dawa zinazoisha muda kabla ya kusambazwa kwa wateja kupungua kutoka Sh4.5 bilioni mwaka 2016/2027 hadi Sh235.84 milioni mwaka 2021/2022 kwa mujibu wa Ripoti za Mdhibiti mkuu na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).
Na ili kuhakikisha dawa zilizoisha pia haziwafikii walengwa Februari mwaka huu aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angela Kairuki ameagiza waganga wakuu wa mikoa na wilaya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhusu dawa ili kuepuka kuwapa watu dawa zilizokwisha muda wake.
Dk Kheri alisema pia uwazi katika utoaji wa taarifa unaofanywa kila baada ya robo taarifa za maandishi zinatolewa kuonyesha usambazaji uliofanyika na kiasi cha fedha kilichobakia.
Maamuzi ndani ya ofisi ya kanda unaongezeka huku akieleza kuwa zamani changamoto zilipowasilishwa kwa meneja wa kanda ya Mtwara aliomba kuziwasilisha makao makuu tofauti na sasa ambapo anaweza kufanyiwa kazi.
Kaimu Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa, Lazaro Msangi alisema kuongezwa kwa idadi ya usambazaji kumetanua wigo wa upatikanaji dawa vituoni.
“Vituo vilikuwa vinakaa baada ya miezi mitatu ndiyo vinapata dawa lakini sasa wanakaa miezi miwili wanapata, kuna wakati tulikuwa tunasubiri kwa muda mrefu na ilisababisha changamoto ndogondogo lakini sasa halipo,” alisema Msangi.