Wakala wa huduma ya maji na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA)Mkoa wa Morogoro imeendelea kutekeleza kwa vitendo agizo la Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi waishio vijijini kwa kutekeleza miradi mbalimbali inayosogeza huduma hiyo karibu na wananchi
Akizungumza kwa niaba ya Kaim Meneja RUWASA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Sospiter Lutonja kwenye ziara ya kamati ya Ufundi na Miradi ya Bodi ya Wakurugenzi RUWASA Mhandisi Shambani Daud amesema kwa Wilaya za Malinyi, Kilombero na Ulanga tayari miradi ya zaidi ya shilingi Bilioni 4 inatekelezwa na wananchi wameshaanza kupata huduma ya maji safi na salama.
Katika Miradi hiyo Mradi wa Mbingu – Igima uliopo Halmashauri ya Mlimba Wilayani Kilombero umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 3.4 na tayari umeanaza kutoa huduma kwa wakazi wa maeneo hayo.
Ngoheranga uliopo Wilayani Malinyi Umegharimu zaidi ya shilingi Milioni mia sita, umeshakamilika ukihudumia zaidi ya watu elfu kumi huku Mradi mwingine Wa Kidugaro kata ya Iragua ujenzi wake umefikia hatua
za mwisho utagharimu milioni mia tatu na kuhudumia wazi elfu 5 hadi elfu tisa.
Amesema lengo la RUWASA ni kuhakikisha kila mwananchi anayeishi kijijini anapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika kama Ilani ya Chama. Cha Mapinduzi 2020/2025 inavyosema.
Mwenyekiti wa kamati ya Ufundi na miradi Bodi ya Wakurugenzi wa RUWASA Mhandisi Ngwisa Mpembe amewataka wakandarasi kukamilisha kwa wakati miradi yote ambayo inatekelezwa ndani ya mkoa wa Morogoro ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.
Aidha amewataka wananchi kutunza miundombinu ya maji katika maeneo yao ili iweze kuwanufaisha watu wengi sambamba na utunzaji wa vyanzo vya maji.
Kwa upande wao wakazi wa maeneo hayo wameishukuru serikali kwa kutekeleza miradi hiyo kwani awali walikua wanapata changamoto kubwa ikiwemo kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo ya maji.
Wamesema licha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji lakini maji hayo hayakuwa safi na salama na kusababisha kupata magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindu pindu.