*Maadhimisho yafanyika kitaifa wilayani Bukombe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, Serikali itaendelea kushughulikia changamoto za Walimu nchini hatua kwa hatua ikiwa ni pamoja na kuwapandisha Madaraja na kutoa malipo ya stahiki mbalimbali.
Rais, Dkt. Samia ameyasema hayo tarehe 6 Oktoba 2023, alipokuwa akizungumza kwa njia ya simu na Walimu zaidi ya 2000 wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita wakati akitoa salamu za Siku ya Walimu Duniani kwa mwaka 2023.
” Walimu ni jeshi kubwa na Serikali inathamini mchango mkubwa mnaoutoa, Serikali itaendelea kufanyia kazi changamoto zenu ili hali zenu ziwe bora zaidi, hivyo nimemwagiza Naibu Waziri Mkuu, Mhe, Dkt Doto Biteko awasikilize kisha aniletee maazimio mliyoyafikia ili niyafanyie kazi” Amesisitiza Mheshimiwa Rais
Mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Walimu Duniani, Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imechukua jitihada mbalimbali ili kuboresha Sekta ya Elimu nchini.
Ametaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kukarabati na kujenga shule mpya ili kukidhi ongezeko la wanafunzi kutokana na mafanikio ya Sera ya Elimu bure ambapo katika mwaka 2022/2023 jumla ya shule mpya 873 zimejengwa.
Pia, ameeleza kuwa, ili kuhakikisha mtoto wa kike anafanya vyema katika masomo ya sayansi na hisabati, Serikali inaendelea na ujenzi wa shule 26 za kitaifa kwa kila Mkoa ambapo shule 10 zimekamilika na zimeanza kupokea wanafunzi wa kidato cha Tano.
Mhe. Mizengo Pinda amempongeza, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko kwa kuonesha kwa vitendo jinsi anavyowajali Walimu na kuwaheshimisha na kueleza kuwa, Walimu hao wanapata faraja kuona kuwa kuna kiongozi anatambua nafasi yao katika jamii katika kujenga nchi na kuwaasa Wabunge wengine kuiga mfano huo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe,
amewaasa wadau wa sekta ya Elimu kuthamini mchango unaotolewa na walimu na kazi kubwa wanayoifanya kwa jamii.
Waziri Biteko ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akikabidhi tuzo maalum kwa walimu waliotoa mchango mkubwa kwenye maisha yake wakati wa safari yake ya kuwa Mwalimu pamoja na Walimu waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali ikiwemo ufaulishaji mzuri wa wanafunzi katika masomo kama vile sayansi na uraia, ubunifu na utunzaji bora wa mazingira,.
Dkt.Biteko ameongeza kuwa, Walimu ndio wazazi, walezi na watoa dira kwenye maisha ya watu wanaowafundisha hivyo wanapaswa kuthaminiwa.
“Nipende kuwashukuru hawa walimu, wamefanya kazi kubwa na kutoa dira ya mwelekeo wa maisha yangu katika kipindi chote nikiwa kwenye chuo cha ualimu cha Katoke” Amesema Dkt. Biteko
Walimu waliopokea tuzo hizo ni pamoja na Mwalimu Justin Temihangwa ambaye kwa sasa ni mstaafu pamoja na Martin Mwombeki ambaye pia ni mstaafu.
Hafla ya siku ya walimu duniani huadhimishwa kila tarehe 5 mwezi wa Kumi kuenzi na kuthamini mchango wa walimu duniani ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni Mabadiliko katika Sekta ya Elimu yanaanza na Mwalimu mwenyewe.
Sherehe hizo za Siku ya Mwalimu zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Juma Kipanga, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba na baadhi ya Wabunge.