Na Mwandishi Wetu,
Mwanza
Wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma
(PSSSF) mkoani Mwanza wameupongeza Mfuko huo kwa kuwa karibu na Wanachama wake
na kuendelea kutoa huduma bora.
Pongezi hizo zimetolewa na Wanachama hao jijini Mwanza Oktoba
5,2023 wakati wa shamrashamra za wiki ya huduma kwa wateja ambayo inaadhimishwa
wiki hii ulimwenguni kote.
Katika kuhakikisha PSSSF inapata mrejesho sahihi kutoka kwa
wanachama wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji Bw. Fotunatus Magambo
aliongoza timu ya maafisa wa PSSSF kuwatembelea wanachama katika ofisi zao na
wastaafu katika makazi yao.
Wakiwa katika ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Jijini Mwanza (MWAUWASA), walikutana na Watumishi watatu ambao wote walisema
wanafurahishwa na huduma za PSSSF.
“Kwa kweli mimi wakati nimejifungua sikupata shida kupata fao la
uzazi, nililipata kwa wakati, hata hivyo nawashauri akina Mama wengine
kuhakikisha wanawasilisha nyaraka zote muhimu ndani ya miezi mitatu baada ya
kujifungua ili waweze kupata fao hilo” alifafanua Bi. Monika Emmanueli,
Mtumishi wa MWAUWASA.
Naye Bi. Vumilia Jonas, Mtumishi MWAUWASA alishauri, “Ni vyema
PSSSF iweke mfumo wa kutoa mrejesho wa Wanachama ili aweze kujua nini
kinaendelea katika huduma anayofatilia”.
PSSSF ina huduma mbalimbali za kumwezesha mwanachama kufuatilia
huduma jambo lolote juu ya uanachama wake, moja ya huduma hiyo ni PSSSF
kiganjani ambapo wanachama anaweza kuhudumiwa kupitia simu janja bila ya
kuhitaji kufika kwenye Ofisi za Mfuko.
Pia Bw. Magambo na timu yake walimtembelea daktari Msataafu wa
hospitali ya wilaya ya Nyamagana, Dkt. Gervas Manzi ambaye anaishi Nyamagana
jijini Mwanza kwa lengo la kumjua hali na kupata mrejesho wa huduma za PSSSF
kwa wastaafu.
“Kwa kweli huduma za Mfuko zipo vizuri, kwa upande wangu nipo
vizuri sana na pensheni yangu naipokea kwa wakati, hata hivyo nashauri PSSSF
iendelee kutoa elimu kwa wanachama ili waweze kujua haki zao kabla na baada ya
kustaafu” alishauri Dkt. Manzi.
Wiki ya huduma kwa wateja huadhimishwa kila wiki ya kwanza ya
Oktoba, lengo lake ni kuzikumbusha taasisi mbalimbali kutoa huduma bora na za
wakati kwa wateja.
Mkurugenzi
wa Mipango na Uwekezaji wa PSSSF Bw. Fortunatus Magambo (wa pili kutoka
kushoto) akiwasikiliza wateja wa PSSSF waliofika katika ofisi za kanda ya ziwa
jijini Mwanza kwa ajili ya kupata huduma. Wa kwanza kushoto ni Bw. Rajabu
Kinande, Meneja wa kanda ya ziwa na wa tatu kutoka kushoto ni Afisa Uhusiano na
Elimu kwa wanachama Mkuu, Bw. Abdul Njaidi.
Mkurugenzi
wa Mipango na Uwekezaji wa PSSSF Bw. Fortunatus Magambo (kushoto) akisalimiana na wateja wa PSSSF waliofika katika ofisi za kanda ya ziwa
jijini Mwanza kwa ajili ya kupata huduma. Wapili kushoto ni Afisa Uhusiano na
Elimu kwa wanachama Mkuu, Bw. Abdul Njaidi.
Nyamagana, Dkt. Gervas Manzi, akizungumza na Watumishi wa PSSSF waliomtembelea
nyumbani kwake jijini Mwanza. Watumishi wa PSSSF,waliongozwa na Mkurugenzi wa
Mipango na Uwekezaji wa PSSSF Bw. Fortunatus Magambo (kushoto) na Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi (kulia)
Mkurugenzi
wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Jijini Mwanza, Bi. Mariam Mshana (katikati) alipokea mfuko wenye makabrasha ya
elimu juu ya PSSSF kutoka kwa Watumishi wa PSSSF wakiongozwa na Mkurugenzi wa
Mipango na Uwekezaji wa PSSSF Bw. Fortunatus Magambo (wa pili kutoka kushoto)
Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo, akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa PSSSF Mwanza baada ya kikao
nao kwa lengo la kuwahamasisha kuendelea kutoa huduma bora kwa wanachama.
Kushoto waliokaa ni Meneja wa kanda ya ziwa, Bw. Rajabu Kinande.