Na Sophia Kingimali
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo katika kulinda na kuendeleza zao la Parachichi wameendelea kulitafutia soko la kimataifa zao hilo na kuendelea kutoa motisha kwa wakulima.
Kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari kutoka idara ya mawasiliano wizara ya kilimo inasema ili kulinda soko la Parachichi nje na ndani ya nchi serikali imeandaa muongozo wa uendelezaji wa zao hilo.
Mnunuzi wa Parachichi anapaswa kuomba kibali wizara ya kilimo kwa kuainisha eneo la uzalishaji atakalonunua na kuambatanisha nyaraka zote muhimu ikiwemo usajili wa kampuni au cheti cha kuandikishwa kama mfanyabiashara binafsi.
Aidha wizara ya kilimo itatoa vibali kwa wanunuzi na kuwatambulisha wanunuzi hao katika ngazi ya mamlaka ya serikali za mtaa kwa ajili ya kupata leseni zinazohusika na ununuzi wa zao hilo ambapo mamlaka hizo ndio zitatoa kibali cha kuvuna na kusafirisha kwa mnunuzi mwenye kibali kilichotolewa na wizara.
Hata hivyo wizara kupitia mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu (TPHPA) ina mamlaka ya kutangaza kufunga au kufungua msimu ununuzi wa zao hilo kwa kuzingatia ukomavu wa tunda hilo.
“Wasafirishaji wa Parachichi kwenda nchi za nje wanapaswa kuzingatia viwango vya ubora vinavyohitajika katika soko husika ikiwa ni pamoja na vifungashio na nyaraka za afya ya mimea”imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Sambamba na hayo mamlaka ya serikali za mitaa zinapaswa kusimamia malipo ya wakulima kulingana na makubaliano baina ya wakulima na wanunuzi wa zao hilo.
Masoko ya parachichi yaliyopo ni pamoja na Indi,Afrika Kusini,China,Uholanzi,Uingereza,
Umoja wa falme za Kiarabu,Kenya,Ufaransa,Ujerumani na Hispania.