Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (wa pili kushoto) akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa mwongozo wa utoaji mikopo ngazi ya stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024 uliofanyika leo Oktoba 4, 2023 katika ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), Profesa Hamis Dihenga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet), Dkt. Adolf Rugayugwa, Rais wa Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Maria John wakiwa katika ofisini za HESLB kwa ajili ya uzinduzi wa mwongozo wa utoaji mikopo ngazi ya stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024 uliofanyika leo Oktoba 4, 2023 katika ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa mwongozo wa utoaji mikopo ngazi ya stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024 uliofanyika leo Oktoba 4, 2023 katika ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), Dar es Salaam.
Rais wa Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Maria John akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa mwongozo wa utoaji mikopo ngazi ya stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024 uliofanyika leo Oktoba 4, 2023 katika ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wakiwa uzinduzi wa mwongozo wa utoaji mikopo ngazi ya stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024 uliofanyika leo Oktoba 4, 2023 katika ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), Dar es Salaam.
…………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Tanzania imezindua mwongozo wa utoaji mikopo ngazi ya stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024 katika fani sita za kipaumbele.
Akizungumza leo Oktoba 4, 2023 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa mwongozo wa utoaji mikopo ngazi ya stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2023/2023, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa kuna kiasi cha Sh 48 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wanaosoma stashahada.
Prof. Mkenda amesema kuwa kiasi hicho kwa ajili ya wanafunzi 8,000 katika maeneo sita ya vipaumbele yenye uhitaji mkubwa wa wataalamu ambayo ni afya na sayansi shirikishi, ualimu wa hisabati, fizikia na mafunzo ya amali, uhandisi na nishati, madini na sayansi ya ardhi na kilimo na mifugo.
Amesema kuwa maeneo hayo ya vipaumbele yamechaguliwa baada ya Serikali kufanya tathmini ya uhitaji mkubwa wa watalaamu katika ngazi ya kati.
“Baada ya kufanya tathmini tumeona tuanze na maeneo haya ili kuwapa fursa vijana wetu kupata ujuzi na kuweza kuajirika baada ya kuhitimu masomo yao,” amesema Prof. Mkenda.
Prof. Mkenda amesema kuwa serikali imejenga hospitali, zahanati na vituo vya afya Serikali pamoja na kukarabati shule ambazo zinahitaji walimu wa sayansi jambo ambalo inatekeleza mageuzi katika sekta za mafuta, gesi, madini na sekta ya kilimo.
Amesema kuwa kutolewa kwa mwongozo huo kutafuatiwa na kufunguliwa kwa dirisha la kupokea maombi kwa njia ya mtandao kwa siku 15 kuanzia Oktoba 7 hadi 22, 2023.
“Niwasisitize waombaji watumie siku nne kusoma mwongozo na kuangalia vigezo ambavyo vimewekwa maana usije ukaona afya ukafikiri kila fani ya afya itatolewa mkopo, kuna maeneo tumeyaangalia” amesema Prof. Mkenda.
Amesema kuwa hasingependa kuona watu wanaostahili wanakosa mkopo kwa sababu ya kushindwa kuzingatia vigezo.
“Muhimu waombaji watambue kuwa baada ya kumaliza masomo wanufaika watarejesha mkopo kwa kiwango cha asilimia 15 kutoka kwenye mishahara yao ya mwezi,” amesema Prof. Mkenda.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet), Dkt. Adolf Rugayugwa amesema mikopo hiyo inaenda kuongeza idadi ya watalaamu katika kada za kati.
Dkt. Rugayugwa amesema wapo vijana wana nia ya kusoma katika ngazi fani mbalimbali lakini wameshindwa kutokana na gharama kubwa kubwa za kulipa ada.
“Tumesubiri kwa muda mrefu suala hili, wanafunzi wa stashahada wakipata mikopo itaongeza idadi ya wanafunzi kwenye kada hii, ambayo ni muhimu katika kutengeneza wafanyakazi” amesema Dkt. Rutayugwa.
Amesema kuwa takwimu kwa wenye shahada ni wengi kuliko wenye stashahada kitu ambacho si kizuri katika utendaji kazi kwani unahitaji mchanganyiko wa kada tofauti.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), Profesa Hamis Dihenga amesema ufuatiliaji wa kina utafanyika kuhakikisha mikopo kwa wanafunzi wahitaji inatolewa kwa ufanisi na kuwafikia walengwa.
Rais wa Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Maria John amewataka wanafunzi wa stashahada kuchangamkia fursa ya mikopo ambayo imekuwa ikiombwa kwa muda mrefu.
“Serikali imetupatia mikopo ili tusome basi twende tukasome ili lengo la kutupa mikopo hii litimie, tupate ujuzi na maarifa tulitumikie taifa na tusisahau tunawajibika kuirejesha mikopo hii na wengine wapate,” amesema Maria.
Mwongozo wa utoaji mikopo ngazi ya stashahada kuanzia mwaka wa masomo 2023/2024 umezinduliwa leo ikiwa ni takribani miezi saba baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kueleza kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kutoa mikopo kwa ngazi hiyo.