Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Pindi Chana akipata maelezo kwa wataalamu wa TEHAMA wa Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamin (RITA) muda mfupi kabla ya kuzindua Mpango wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri wa miaka chini ya miaka mitano katika Mkoa wa Kigoma jana ambako watoto zaidi 396,182 wanatarajiwa kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza wa Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamini mara baada ya kuzindua Mpango wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri wa miaka chini ya miaka mitano katika Mkoa wa Kigoma jana ambako watoto zaidi 396,182 wanatarajiwa kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.
……………………………..
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Balozi Dk Pindi Chana amefurahishwa na mafanikio ya utekelezaji wa mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan wa kusajili watoto wote chini ya miaka tano na kupatiwa vyeti ya kuzaliwa bure.
“Kwa namna ya pekee na niaba ya serikali nachukua nafasi hii kuipongeza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), wadau wa usajili na utambuzi, ofisi za wakuu wa mikoa yote ambayo mpango huu unatekelezwa kwa kutuletea matokeo haya makubwa yaliyopatikana,” alisema Dk Chana.
Akizindua Mpango wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri wa miaka chini ya miaka mitano katika Mkoa wa Kigoma ambako watoto zaidi 396,182 wanatarajiwa kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa, Waziri Chana amewataka wana Kigoma kuchangamkia fursa hiyo ya adhimu kujitokeza na kuwasajili watoto.
Alichukuwa fursa hiyo pia kuwashukururu wadau wa maendeleo kwa kufanikisha utekelezaji wa mpango huo likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la linalohudumia Watoto (UNICEF), Serikali ya Canada, Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR), Kampuni ya Mawasiliano ya TIGO pamoja na wadau wengi kwa kuendelea kuwa sehemu ya mpangon huu muhimu.
“Cheti cha kuzaliwa ni haki ya kila mtoto aliyezalizwa katika ardhi ya Tanzania bila kujali uraia wa wazazi wake.Serikali kupitia RITA na wadau mbalimbali wa usajili na utambuzi wameweka utaratibu ambao watoto na wazazi wao wanatambuliwa,” alisema.
Aidha, Dk Chana amewataka watendaji kata na wahudumu wa vituo vya afya kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo wa hali ya juu kwa kuweka mbele maslahi ya taifa.
“Usajili ni suala muhimu kwa usalama wa nchi kwa hiyo, masharti na vigezo vilivyowekwa lazima vizingatiwe. Nawaasa pia watendaji kutunza vitendea kazi,” alisema .
Awali, akimweleza waziri Chana kabla ya kuuzindua mpango huo jana, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi alisema tangu mpango huo uzinduliwe juni 2013 zaidi ya watoto 8,646,324 wameshasajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa katika mikoa 24 ambako mpango huu umetekelezwa.
“Mpango huu uliouzindua leo(Jana) umeleta maboresho sambamba na kusogeza huduma za usajili karibu na maeneo ya makazi ya wananchi hiyo huduma ya usajili kutolewa katika vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya mama na mtoto na ofisi za watendaji kata,” alisema Kanyusi.
Alisema kupitoa mpango huu, huondoa ada ya cheti kwa watoto wanaosajiliwa sambamba na kuimarisha matumizi ya TEHAMA ambapo simu za kiganjani iliyokwekwa program maalumu kutumika kuingiza na kutuma taarifa kwenda kanzidata ya wakala.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye alisema takwimu zinaonyesha wastani wa asilimia 10.5 tu ya watoto wote mkoani humo wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.
“Tunaishukuru serikali kwa kushirikiana na wadau kwa kutekeleza mpango huu kwani kila mtoto mtoto chini ya umri wa miaka mitano ataweza kusajiliwa na kupata cheti za kuzaliwa bure,” alisema RC Andengenye.