*Mara*
Kundi lingine la Watumishi wapatao 14 kutoka kada mbalimbali za Wizara ya Madini ikihusisha Makatibu Mahususi, Watunza Kumbukumbu na Wahudumu wametembelea Mgodi wa North Mara uliopo Mkoani Mara.
Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa kutembelea migodi katika utekelezaji wa maazimio na ahadi alizotoa Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo lililofanyika mwezi Mei, 2023, jijini Dodoma ambapo kundi la kwanza lilitembelea migodi mwezi Agosti mwaka huu.
Aidha, ziara hiyo inalenga kuwajengea uelewa wa pamoja watumishi wote wa Wizara kuhusu shughuli zinazofanywa katika Sekta ya Madini hususan shughuli za uchimbaji wa madini katika migodi mikubwa, ya kati na midogo ili kuwezesha malengo mahususi ya wizara kutekelezwa kwa pamoja kama familia moja ya Madini.
Watumishi hao wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali katika mgodi huo ikiwemo mgodi wa chini ( underground mining), sehemu ya uchenjuaji (processing plant) bwawa la huifadhi tope sumu ( TSF) , sehemu ya upokeaji na utunzanji wa vifaa vinavyotumika katika mgodi pamoja na kutembelea miradi ya jamii inayotekelezwa na migodi hiyo kupitia Mpango wa Uwajibikaji wa Migodi kwa Jamii (CSR).
Hili ni kundi la pili la watumishi wa kada hizo kutembelea maeneo ya migodi ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa.