Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS) katika Kijiji cha Maziwa ng’ombe Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
…….
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa wiki mbili kwa Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba kukamilisha taratibu za zabuni na ununuzi wa pampu, mashine za umeme wa jua na matanki ya kuhifadhia maji ili huduma ya maji safi iweze kuwafikia wananchi wa Kijiji cha Maziwa ng’ombe.
Ametoa agizo hilo baada ya kutembelea na kukagua Mradi wa kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS) ukihusisha ujenzi wa matuta ya kuzuia maji ya bahari kuingia katika mashamba ya mpunga, upandaji wa miti ya mikoko, matumizi ya majiko banifu na ukaguzi wa visima vya maji.
“Kuna mambo tukiyafanya tunapoteza imani kwa wananchi, wananchi hawa wanataka maji waanze kutumia sasa nakupa muda wa wiki mbili mkakae hivyo vikao vya zabuni na mkamilishe huo mchakato, sisi wote hapa tunaendeleza na kutekeleza azma ya viongozi wetu wakuu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambao wamekuwa wakipeleka huduma kwa wananchi sasa sisi wengine hatuna sababu ya kuchelewesha huduma mbalimbali kwenda kwa wananchi na tayari fedha ya mradi huu ishatoka,kwanini wananchi hawapati maji,“ amesema Mhe. Khamis Wakizungumza wakati wa ziara hiyo wananchi wa Kijiji cha Maziwa ng’ombe wamesema wamekua wakipata maji kila mwisho wa mwezi hali inayowapelekea kutumia gharama kubwa na umbali mrefu kufuata maji huku gharama hizo kubwa zikiendelea kuwasababishia hali ngumu ya maisha huku wakimuomba Naibu Waziri Khamis kutatua kero hiyo kupitia mradi huo.
Mradi huo wa visima hivyo vya maji katika Kijiji cha Maziwa ng’ombe vipo katika hatua ya zabuni kwa ajili ya ufungaji wa pampu,mashine za umeme wa sola na matanki ya maji ambayo Naibu Waziri Khamis ametoa muda wa wiki mbili ili mchakato huo wa zabuni ukamilike.
Mradi wa LDFS pia unatekelezwa katika wilaya za Magu (Mwanza), Nzega (Tabora), Mkalama (Singida) na Kondoa (Dodoma) ambapo gharama yake kwa ujumla ni shilingi bilioni 15.