Na Sophia Kingimali
MAKAMU wa Rais Dk.Philip Mpango amemtaka Waziri wa Uchukizi Profesa Makame Mbarawa kufanya uchambuzi wa gharama za Usafirishaji wa mizigo katika ndege ya mizigo ndani ya siku 14.
Pia amesema serikali haitovumilia uzembe wowote utakaojitokeza tena ndani ya Shirika la Ndege Tanzania
( ATCL)kama ilivyowahi kuwa ndani ya miaka ya nyuma.
Maagizo hayo ameyatoa jijii Dar es Salaam Oktoba 3 wakati wa mapokezi ya ndege aina ya B 737- Max 9 yenye uwezo wa kubeba abiria 181na kuzindua ndege nyingine mbili za mafunzo kwa wanafunzi wa chuo Cha Usafirishaji Tanzania(NIT).
Dk.Mpango amesema amepokea changamoto za gharama kubwa ya usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi katika viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro na Abeid Aman Karume Zanzibar ikilinganishwa na viwanja vya nchi jirani.
Amewataka Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Fedha washirikiane na wenzao wa Zanzibar ili kuchambua na kubaini kiini cha changamoto hiyo na kupendekeza hatua zinazopaswa kushughulikiwa.
“Tazameni hizo tozo na kodi mbalimbali, ikiwemo ‘Navigation, Fees’ mfanye uchambuzi wa uhakika ndani ya siku 14 kuanzia leo na mlete mapendekezo serikalini”amesema.
Amesema serikali imewekeza fedha nyingi kununua ndege hizi na katika kuboresha viwanja vya ndege lengo likiwa kuhakikisha shehena kubwa ya mizigo inapatikana kuongeza Pato la taifa.
Pia ameilekeza Wizara ya Uchukuzi pamoja na Bodi ya wakurugenzi na wafanyakazi wa ATCL kutimiza wajibu wao wa kusimamia vizuri utoaji wa huduma za usafiri wa anga ili kuimarisha ushindani kikanda na kimataifa ili kuongeza mchango katika pato la Taifa
Aidha amewataka kufanya kazi kibiashara kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta hiyo.
“Bado kuna malalamiko ya wateja wa ATCL kuhusu huduma za usafiri ikiwemo kuahirisha safari au kusogeza mbele muda wa kusogeza safari, na kuna kelele nyingi sana hivyo baada ya kupokea ndege hiyo matarajio ya watanzania ni kuwa sasa ATCL watamaliza kabisa kero hiyo,”amesema
Pia ameitaka Wizara ya Uchukuzi kufuatilia kwa ukaribu ubora wa huduma zinazotolewa na shirika la ATCL na kuhakikisha bidhaa zinauzwa ndani ya ndege hiyo ziwe zinazozalishwa nchini na kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania(TBS) ili kukuza kipato na wajasiliamaki wa kitanzania.
Vilevile ameitaka Bodi ya ATCL kulisimamia vizuri shirika hilo ili kulinda mtaji uliowekezwa na serikali kwa niaba ya Watanzania.
Katika hatua nyingine Dk. Mpango amesema ameridhishwa na hatua iliyofikia katika utekelezaji wa makubaliano ya awali ikiwemo kufanya tathmini ya awali ya kitaalamu ili kuandaa mkataba wa usanifu wa ujenzi pamoja na tathmini ya sampuli za udongo kutoka eneo la mradi.
Kutokana hilo ameitaka Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha kazi zote za awali zilizopangwa zinakamilika itakapofika Februari,mwakani.
“Hivi sasa mradi wa uboreshaji na upanuzi wa jengo la pili la abiria katika kiwanja Cha Julius Nyerere uweze kuanza rasmi na ninauelekeza uongozi NIT, marubani wakufunzi na marubani wanafunzi wakazitunze ndege hizo ambazo zinanunuliwa kwa ajili ya kufundishia marubani ili ziweze kudumu na kuendelea kufundishia marubani walio wengi zaidi,” amesema.
Pia amemuelekeza Profesa Makame Mbarawa kuangalia chuo Cha NIT kibajeti kuanzia mwaka ujao wa fedha ili maombi yao ya ndege nyingine mbili ambazo zina Injini mbili ziweze kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameahidi kutekeleza majukimu yake kwa ufanisi kwa maslahi ya nchi.
Amesema ndege hiyo inaongeza mtandao wa biashara kati ya ATCL na nchi nyingine na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Pia ametangaza kiwanja cha ndege cha Dodoma kuanza rasmi kufanya kazi Kwa saa 24 kuanzia leo huku wakiweka mkakati wa kuweka taa katika viwanja vya Iringa na Songea kuviwezesha kufanya kazi kwa saa hizo.
Akizungumza baada ya kuwasili Kwa ndege hiyo, Mtendaji Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijengea ATCL kutoa huduma shindani nchini.
Ndege iliyowasili inauwezo wa kubeba abiria 181 ni ya masafa ya kati na kuruka kwa saa nane bila kutua.
Kuwasili Kwa ndege hiyo kunaiwezesha ATCL kuwa na ndege 14 hivyo amewataka wanatanzania kujiandaa kupokea ndege nyingine mbili kabla ya mwishoni mwa mwaka huu.
“Katika mwaka wa fedha 2016-2017 ATCL ilipokea abiria 106,138 na mwaka 2021-2028 walikuwa milioni 1.7, mapato yaliyopatikana mwaka 2022-2023 ni Sh. Bilioni 372.8 na kupitia ndege ya mizigo kuanzia Juni mwaka huu ilibeba Tani 337 huku matarajio yakiwa Tani 468,”alisema
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Usafirishaji Tanzania(NIT),Profesa Zakaria Mganilwa, amesema serikali imekuwa inathamini mchango wa sekta ya Usafirishaji nchini.
Profesa Mganilwa amesema Tanzania Bado inakabiliwa na chagamoto ya uhaba wa wataalamu wa ndege kwani wanaorusha ndege kubwa nchini ni 304 ambapo wazawa ni asilimia 43 tu.
Amesema ndani ya wiki mbili baada ya kuleta ithibati wataanza kutoa kozi ya urubani kwa sababu walikuwa wakisubiria ndege za mafunzo ambazo zimepatikana mbili.
Amesema utoaji wa mafunzo ya ndege nchini utapunguza gharama kwa asilimia 50 kwa watanzania kwenda kusoma nje ya nchi.
“Tunaomba serikali inunue ndege nyingine mbili ili zitusaidie kufudisha wanafunzi 20 kwa mara moja kwa sababu Watanzania wanaohitaji kusoma kozi ya urubani ni wengi na tunaomba tuongezwe wakufunzi,”amesema.