Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam kuongoza mapokezi ya ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 iliyowasili leo tarehe 03 Oktoba 2023. Kushoto ni Mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango.
Ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 yenye uwezo wa kupakia abiria 181 ikiwasili nchini kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam.na kumwagiwa maji (water salute) leo tarehe 03 Oktoba 2023.
Ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 yenye uwezo wa kupakia abiria 181 Ikimwagiwa maji (water salute) mara baada ya kuwasili nchini kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Oktoba 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa hafla ya kupokea ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam. (tarehe 03 Oktoba 2023).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Naibu Spik awa Bunge la Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango pamoja na viongozi wengine wakati akikata utepe kuashiria kupokea ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 iliyowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Oktoba 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Mkewe Mama Mbonimpaye Mpango katika ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 mara baada ya kuipokea ilivyowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Oktoba 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa amekaa katika chumba cha marubani kwenye ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Oktoba 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa amekaa katika chumba cha marubani kwenye ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Oktoba 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka, mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango pamoja na viongozi wengine katika picha ya pamoja mara baada ya kupokea ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Oktoba 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakishuka katika ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 mara baada ya kuipokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Oktoba 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na marubani pamoja na watumishi wa shirika la ndege nchini ATCL mara baada ya mapokezi ya ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737- MAX9 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Oktoba 2023.
….
Mabibi na Mabwana. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!Napenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia uhai na kutukutanisha hapa.
Awali, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye aliyealikwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hii muhimu ya mapokezi ya ndege yetu mpya ya abiria ya masafa ya kati aina ya Boeing 737-9MAX, pamoja na uzinduzi wa ndege mbili aina ya Cessna 172S kwa ajili ya mafunzo ya Urubani katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Mheshimiwa Rais yuko nje ya nchi akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano na Maonesho ya kimataifa ya bidhaa za bustani (International Horticultural Expo 2023, Doha, Qatar) katika Jiji la Doha, Qatar na baadaye kwenye ziara ya Kiserikali nchini India.
Dhumuni kubwa ni kutafuta masoko ya bidhaa zetu za mbogamboga na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu na nchi ya India katika masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano, maji, afya na viwanda.
Kutokana na majukumu hayo ameshindwa kujumuika nanyi, hivyo amenituma mimi kumwakilisha na ninamshukuru sana kwa heshima hii kubwa.
Aidha, naomba viongozi na wananchi wote tuungane kumpongeza Kiongozi wetu Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa makofi na vigelegele kwa kutuletea ndege nyingine kubwa, baada ya kushusha ile ndege kubwa mpya ya mizigo mwezi Juni mwaka huu.
Napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa (Mb.) na Watendaji wa Wizara ya Uchukuzi kwa maandalizi mazuri ya hafla hii. Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi;Sekta ya Uchukuzi na Usafiri wa anga ni miongoni mwa vichocheo muhimu vya uchumi na maendeleo.
Shirika letu la Ndege limechochea ukuaji wa uchumi kwa kuwezesha usafirishaji wa bidhaa zetu kwa haraka na usalama hususan zile za thamani na zinazoharibika haraka kama vile matunda, mbogamboga, samaki, maua, nyama na nyinginezo. Aidha, uwezo wetu wa kuwasafirisha watalii wanaokuja nchini umeongezeka.
Hii inathibitishwa na takwimu zilizotolewa hapa zinazoonesha ongezeko la vituo na idadi ya watu wanaosafiri kwa Ndege za ATCL kutoka abiria 106,138 mwaka 2016/17 (sawa na 24% ya umiliki wa soko la ndani kwa safari zenye ratiba maalum) hadi kufikia abiria 1,070,734 mwaka 2022/23 (sawa na 53% ya umiliki wa soko lote la ndani).
Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi;Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya Uchukuzi. Hii ni pamoja na kuendelea kutengeneza mazingira mazuri na shindani ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.
Hivyo, kuwasili kwa ndege hii ya kisasa ambayo inafanya idadi ya ndege katika Shirika letu kufikia 14 ni sehemu ya Mkakati wa Serikali wa kuendelea kuiwezesha ATCL kutoa huduma bora na ya ushindani, huku ndege mbili zaidi, Boeing 737 Max 9 na Boeing 787-8 Dreamliner, zikitarajiwa kuwasili nchini kati ya mwezi Oktoba na Desemba 2023 na mwezi Machi 2024.
Mheshimiwa Rais, amejizatiti kuhakikisha Sekta ya Uchukuzi inaimarika na anafanya haya yote kwa kutambua kuwa, ufanisi katika huduma za uchukuzi utaliweka Taifa letu kwenye nafasi nzuri ya ushindani wa kibiashara, kutuongezea mapato ya fedha za kigeni na kukuza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa.
Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi;Pamoja na mapokezi ya ndege hii kubwa ya masafa ya kati, pia tutazindua ndege mbili za mafunzo za Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, aina ya Cessna 172S ambazo zitatumika katika mafunzo ya Urubani.
Mwaka 2021, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan iliiwezesha NIT kuingia mkataba wa ununuzi wa ndege mbili za mafunzo ya Urubani aina ya Cessna 172 Skyhawk, zinazotumia injini moja kutoka Kampuni ya Textron Aviation Inc. ya Marekani.
Kama ilivyoelezwa hapa, ndege hizo zitatumika katika mafunzo ya Urubani – Daraja la Awali (Prívate Pilot Licence- PPL) yanayochukua miezi 6 na mafunzo ya Urubani wa Biashara (Commercial Pilot Licence-CPL) yanayochukua miezi 12. Serikali imetoa fedha za kukiimarisha Chuo cha NIT ili kiweze kutoa mafunzo ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege, Uendeshaji wa Safari za Ndege pamoja na Uhudumu wa Ndani ya Ndege kwa Ithibati za TCAA. Lengo ni kuzalisha wataalam wengi katika soko la ajira watakaohudumu katika mashirika mbalimbali ya ndege, ikiwemo ATCL.
Aidha, ili kuongeza ufanisi wa NIT katika kutoa mafunzo ya Urubani, mwezi Juni, 2023, Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha NIT kuingia mkataba wa ununuzi wa ndege moja mpya ya mafunzo yenye injini mbili aina ya Beechcraft Baron G58 toka Kampuni ya Textron Aviation Inc. ya Marekani.
Ndege hiyo inatarajia kuwasili katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Hivyo, naelekeza Bodi ya Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kuhakikisha kuwa ndege hizo zinazonunuliwa kwa fedha nyingi za Umma zinatunzwa kwa kuzingatia masuala ya usalama ili ziweze kutumika kutoa mafunzo kwa muda mrefu zaidi. Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi;Kwa kutambua fursa zilizopo katika soko la usafiri wa anga na mchango wake katika ukuaji wa uchumi, Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ndogo ya usafiri wa anga ikiwemo ujenzi wa viwanja vya ndege na kuweka mifumo na mitambo ya kisasa ya rada za kuongozea ndege na kulifanya anga la Tanzania kuwa salama.
Halikadhalika, kukamilika kwa ufungaji wa taa za kuongozea ndege katika viwanja vya ndege vya Dodoma na Songwe ni hatua nyingine muhimu itakayowezesha ATCL kuongeza wigo wa safari zake za ndani kwa kuanzisha safari za usiku katika viwanja hivyo.
Aidha, Serikali imefikia hatua ya kuridhisha kuelekea kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa uboreshaji na upanuzi wa jengo la pili la abiria katika kiwanja hiki cha JNIA, kwa mkopo kutoka Serikali ya Ufaransa.
Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi;Ili kuwezesha sekta ndogo ya usafiri wa anga kuleta tija kwa Taifa letu, napenda kusisitiza yafuatayo:Kwanza, kuhusu uratibu na usimamizi mzuri wa huduma za usafiri wa anga.
Naelekeza Wizara ya Uchukuzi, Bodi ya Wakurugenzi na Wafanyakazi wa ATCL kutimiza wajibu wenu wa kusimamia vizuri utoaji huduma za usafiri wa anga ili kuimarisha ushindani wetu Kikanda na Kimataifa na hivyo kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa. Fanyeni kazi kibiashara na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia sekta hii. Niwakumbushe kuwa, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020), Ibara ya 58 (a) na (h) (i-ii)) inatutaka kuliimarisha Shirika letu la ATCL na Sekta ya Usafiri wa anga kwa ujumla.
Tuhakikishe tunafikia na kuvuka malengo yaliyowekwa katika Ilani.Kwa mfano, bado kuna malalamiko ya wateja wa ATCL kuhusu huduma za usafiri, ikiwemo kuahirisha safari au kusogeza mbele muda wa kuanza safari (kiwanja cha Mwanza na vingine).
Mheshimiwa Waziri, baada ya kupokea ndege hii mpya, matarajio ya Watanzania ni kuwa ATCL sasa watamaliza kabisa kero hiyo ya kuahirisha au kufuta safari. Wizara ya Uchukuzi ifuatilie kwa karibu ubora wa huduma zinazotolewa na ATCL.
Aidha, ni vema idara ya ununuzi wa vyakula na viburudisho ndani ya ndege za ATCL ihakikishe inatoa kipaumbele kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ambazo zimethibitishwa na TBS, ili kukuza kipato na ajira za wajasiriamali/wazalishaji wa Tanzania.
Pili, naisisitiza Bodi ya ATCL kulisimamia vizuri Shirika hili ili kulinda mtaji uliowekezwa na Serikali kwa niaba ya Watanzania.
Serikali haitavumilia uzembe wowote utakaojitokeza tena ndani ya ATCL kama ilivyowahi kuwa miaka ya nyuma. Tatu, nimepokea changamoto ya gharama kubwa ya usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi katika viwanja vyetu vya JNIA, KIA na Abeid Amani Karume, Zanzibar ikilinganishwa na viwanja vya ndege vya nchi jirani na gharama za kusafirisha mizigo (general cargo) kwa kutumia ndege za mashirika mengine ya Ndege duniani. Naielekeza Wizara ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Fedha washirikiane na wenzao wa Zanzibar ili kuchambua na kubaini kiini cha changamoto hii, na kupendekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa. Serikali imewekeza fedha nyingi kununua ndege na katika kuboresha viwanja vya ndege na miundombinu yake, ili kuhakikisha shehena kubwa ya mizigo inapatikana na hivyo kuongeza mapato.
Hivyo, fanyieni kazi suala hili na kuwasilisha taarifa kwa Mamlaka (SMT na SMZ) ndani ya siku 14 kuanzia leo.Nne, nimeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa makubaliano ya awali ikiwemo kufanya tathmini ya awali ya kitaalam ili kuandaa mkataba wa usanifu wa ujenzi na tathmini ya sampuli za udongo kutoka eneo la mradi.
Ninaitaka Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha kuwa kazi zote za awali zinakamilika ifikapo mwezi Februari 2024, ili mradi wa uboreshaji na upanuzi wa jengo la pili la abiria katika kiwanja hiki uweze kuanza rasmi.
Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa na Ndugu Wananchi;Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwahakikishia kuwa Serikali imedhamiria kuinua na kuboresha usafiri wa anga.
Hivyo, nawahimiza wananchi kuendelea kuliamini na kulitumia Shirika letu la Ndege (ATCL) ambalo lina ndege za kisasa na linatoa huduma bora na zenye ushindani.
Vilevile, nawashukuru sana Wananchi wa Mikoa ya Da es Salaam na Pwani kwa kujitokeza kwa wingi sana kuipokea ndege yetu na kushiriki uzinduzi wa ndege mbili za mafunzo za Chuo cha Taifa cha Usafirishaji. Baada ya kusema haya, sasa niko tayari kuipokea ndege yetu mpya aina ya Boeing 737-9MAX na kuzindua ndege mbili za mafunzo za NIT aina ya Cessna 172S.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA…!ASANTENI KWA KUNISIKILIZA!