Mfanyakazi wa Kampuni ya kikandarasi ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCEC) akiendelea na hatua ya ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje, jijini Dodoma (Dodoma Outer Ring Road) huku akiwa amevaa vifaa vya usalama mahala pakazi, leo tarehe 3 Oktoba ,2023.
Wafanyakazi wa kampuni ya kikandarasi ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCEC) wanaojenga barabara ya mzunguko wa nje, jijini Dodoma wakiwa wamevaa vifaa vya usalama wakati wa kazi kufuatia agizo lililotolewa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa tarehe 29 Septemba, 2023 la kumtaka Mkandarasi huyo kuwapa mafundi hao vifaa vya usalama.
Mhandisi Alinanuswe Mwakiluma wa Wakala wa Barabara (TANROADS ), jijini Dodoma akitoa maelezo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), kufuatia utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa la kumtaka mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCEC) anaetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje, jijini humo kuwapa mafundi vifaa vya usalama.
Mwakilishi wa Mkandarasi kutoka kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCEC), Mha. David Kapinga, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), kufuatia utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa la kumtaka mkandarasi huyo anaetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje, jijini humo kuwapa mafundi vifaa vya usalama.
…..
Wakala wa Barabara (TANROADS) jijini Dodoma, umesema kuwa utahakikisha unaendelea kusimamia utekelezaji wa masuala ya usalama kwa wafanyakazi wanaotekeleza miradi ya Sekta ya Ujenzi katika miradi yote nchini.
Hayo yamesemwa na Mhandisi Alinanuswe Mwakiluma, kwa niaba ya Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Mha. Leonard Chimagu, leo tarehe 3 Oktoba, 2023 jijini humo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na agizo la Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, alilolitoa wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje (Km 112.3) jijini humo tarehe 29 Septemba, 2023 kwa Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCEC) na kukuta baadhi ya wafanyakazi wamevaa viatu vilivyochanika.
Mhandisi Mwakiluma, amesema kuwa jukumu la Wakala huo ni kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi anapatiwa vifaa mbalimbali vya usalama kwa mujibu wa mkataba ili kumlinda wakati wa changamoto yoyote inapoweza kujitokeza mahala pakazi.
“Nadhani mmeshuhudia wenyewe, wafanyakazi wa Mkandarasi huyu tayari wamepewa vifaa vya usalama ikiwemo kofia ngumu, viatu, barakoa na kiakisi mwanga (reflector), kwa hiyo sisi kama TANROADS mtaona ni namna gani tulivyoweza kufuatilia na kutekeleza agizo la Waziri, amesema Mha. Mwakiluma.
Ameongeza kuwa TANROADS itahakikisha inaendelea kutekeleza maelekezo ya Waziri huyo kuhusiana na suala hilo hata kwa makandarasi wengine wanaoendelea kutekeleza miradi ya ujenzi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkandarasi kutoka kampuni ya CCEC, Mha. David Kapinga, amesema kuwa jumla ya vifaa 50 vimebadilishwa, na kampuni yao imekuwa ikigawa vifaa vya usalama kila baada ya miezi mitatu ila baada ya agizo la Waziri Bashungwa kwa sasa utaratibu utabadilishwa na kugawa vifaa vingine mara tu vya awali vitakapokuwa vimeharibika.
Naye, Innocent Isaka, akizungumza kwa niaba ya Wafanyakazi wa Kampuni ya kikandarasi ya CCEC amesisitiza kwa wakandarasi kuendelea kutoa vifaa kwa wafanyakazi pindi vinapoharibika na kutoa rai kwa wafanyakazi kuwa waaminifu na kuvitunza vifaa hivyo ambavyo vinapunguza vihatarishi katika maeneo ya kazi.
Tamimu Budi, ameishukuru kampuni yao kwa kuweza kutekeleza agizo la Waziri kwa wakati na amesisitiza kuendelea kufanya hivyo kwani vifaa hivyo vinawapa hamasa na utambuzi hata wakati wa usiku Mradi wa Barabara ya Mzunguko wa nje ya Dodoma (Km 112.3), unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi Bilioni 221 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2024.