…………………..
Na Sixmund Begashe -Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) imeshika nafasi ya pili katika tuzo ya utendaji bora na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kama sehemu ya mchango wake katika uwezeshaji wananchi kiuchumi na utendaji bora wa mfuko huo.
Kabla ya kutoa tuzo hizo kwenye kongamano la saba la uwezeshaji wananchi kiuchumi Jijini Dodoma, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amezipongeza Taasisi na Sekta zote binafsi zinazo jishughulisha na uboreshaji wa maisha ya wananchi kiuchumi na kuwa kwa kufanya hivyo ni kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya Maliasili na Utalii ili kujiendeleza kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Katibu Tawala Mfuko wa Misitu Tanzania, Dkt. Tuli Salum Msuya amechukua fursa hiyo kuishukuru NEEC kwa kutambua mchango wa TaFF katika kuwezesha wananchi kiuchumi na kutambua utendaji bora wa mfuko huo hali iliyopelekea kupewa tuzo.
Dkt. Msuya ameendelea kusema kuwa tuzo hiyo ni kichocheo cha utendaji kazi zaidi kwa mfuko wa TaFF katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na fursa zilizopo katika sekta ya Misitu na kuchangia zaidi katika pato Taifa kwa ujumla.
Aidha Dkt. Msuya ameongeza kuwa TaFF hutoa ruzuku kwa lengo la kuwezesha miradi ya kuboresha uhifadhi, uendelezaji na usimamizi wa rasilimali misitu hapa nchini.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bibi Beng’i Issa amesema lengo la kongamano hilo la 7 pamoja na mambo mengine ni kuwaleta wadau pamoja ili kupeana uzoefu ikiwemo kutambua mchango wa sekta binafsi na taasisi mbalimbali za umma hapa nchini.