Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga akiwa katika ziara leo Oktoba 2, 2023 ya kukagua kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gasi asilia cha Tegeta Gas Plan, Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga (wa kwanza kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo Hanga wakati akiwasili katika Kituo Cha kuzalisha umeme kwa kutumia gasi asilia cha Tegeta Gas Plan, Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na wafanyakazi wa Shirika hilo akikagua mitambo ya kuzalisha umeme katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gasi asilia cha Tegeta Gas Plan, Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga akizungumza na waandishi habari leo Oktoba 2, 2023 baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi katika Kituo Cha kuzalisha umeme kwa kutumia gasi asilia cha Tegeta Gas Plan, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo Hanga akizungumza na waandishi habari leo Oktoba 2, 2023 katika Kituo Cha kuzalisha umeme kwa kutumia gasi asilia cha Tegeta Gas Plan, Dar es Salaam.
Baadhi ya Mitambo ya kuzalisha umeme katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gasi asilia cha Tegeta Gas Plan, Dar es Salaam.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Wizara ya Nishati imesema hali ya uzalishaji wa umeme imeimarika baada ya mitambo ya kufua umeme katika kituo cha kufua umeme Ubungo I na II iliyokuwa imepata hitilafu ambapo kwa sasa imeanza kufanya kazi.
Akizungumza leo Oktoba 2, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati akikagua kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gasi asilia cha Tegeta Gas Plan, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa ametoa maelekezo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha matangenezo ya lazima ya mitandao iliyopata hitilafu inakamilika kwa wakati ili kuimarisha huduma ya umeme.
Mhe. Kapinga amesema kuwa inapotokea hitilafu TANESCO wahakikishe matengenezo yanafanyika haraka ili huduma ya umeme iendelee kupatikana.
“Hatutakubali watanzania walale bila umeme kwa sababu ya changamoto ndogo ndogo ikiwemo kuharibika kwa Transfomer, mita, kukatika kwa wire ya umeme, naomba TANESCO mfatili kuhakikisha umeme unapatikana ndani ya muda mfupi” amesema Mhe. Kapinga.
Mhe. Kapinga amesema kuwa katika kituo cha kuzalisha umeme cha Tegeta Gas Plan uzalishaji wa umeme unaendelea kupitia mitambo mitano ambayo inazalisha megawatt 43.
Amesema kuwa kwa sasa mitambo minne inaendelea na uzalishaji wa umeme katika kituo cha Tegeta Gas Plan, huku akieleza kuwa mtambo mmoja mafundi wanaendelea matengenezo ya lazima.
“Lengo ni kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana, tutahakikisha kila mtanzania anapata umeme, hivyo wakati umefika kwa TANESCO kuunganisha umeme sehemu zote ambazo kuna miundombinu’’ amesema Mhe. Kapinga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo Hanga, amesema kuwa TANESCO kwa kushirikana na Wizara ya Nishati inaendelea kufanya juhudi kadri inavyowezekana ili kuhakikisha umeme wa kutosha unapatikana kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kijamii na uzalishaji mali.
Amesema kuwa wanaendelea na jitihada mbalimbali ili kufikia malengo “Tunapokea kila aina ya ushauri ambao tunaona unaweza ukafaa, lengo umeme upatikane kwa gharama ambayo wananchi wanaweza kumudu”
Mhandisi Gissima Nyamo Hanga ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika sekta ya nishati kwa ajili ya kuhakikisha wanazalisha umeme wa kutosha.