Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI wa Wilaya ya Dodoma wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kuupokea, kuushangilia na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 utakaoingia wilayani Dodoma kesho tarehe 3 Oktoba, 2023.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Dodoma ofisini kwake.
Alhaj Shekimweri alisema “nipende kuwafahamisha kuwa Mwenge wa Uhuru kesho tarehe 3 Oktoba, 2023 utapokelewa Wilaya ya Dodoma. Tunatarajia kuupokea Mwenge wa Uhuru pale Makutopora saa 12 asubuhi ukitokea Wilaya ya Kondoa. Utaendelea kukimbizwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma ukikagua, kuzindua na kuweka jiwe la msingi katika miradi ya maendeleo. Wananchi wote mjitokeze kuulaki na kuushangilia Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Dodoma”.
Akiongelea ratiba ya Mwenge wa Uhuru alisema kuwa Mwenge wa Uhuru utashiriki kupanda miti na ujumbe wa Mwenge Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini, kisha utakwenda kuweka jiwe la msingi shule ya mchepuo wa kiingereza ya Dodoma iliyopo eneo la Ilazo. Eneo lingine ni kuweka jiwe la msingi mradi wa Barabara Nzuguni- Mahomanyika kisha kuelekea mradi wa Maji safi Nzuguni kuweka jiwe la msingi.
Mwenge wa Uhuru utakagua shughuli za club ya wapinga rushwa na dawa za kulevya katika Chuo cha Veta. Shughuli nyingine ni kuzindua Kituo cha Afya Nkuhungu na kutembelea kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Vijana Faru.
“Nichukue nafasi hii kwa niaba ya viongozi wenzangu ngazi ya wilaya na wapenda maendeleo na wadau wote kuwaalika kushiriki kuanzia mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na kumpokea mzalendo Abdalla Kaim Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 na kushirikiana nasi kwenye ukaguzi wa miradi na hatimae kuja kwenye eneo la mkesha ambapo tutapokea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru” alisema Alhaj Shekimweri.
Kutakuwa na uchangiaji wa damu na upimaji wa vvu na malaria. “Tumeandaa sherehe kubwa baada la risala ya utii ambapo kutakuwa na mkesha wa Mwenge wa Uhuru tumealika wasanii wengi pamoja na Sholo Mwamba, Dulla Makabila, Moni Centrozone, Bushoke, Madee na wasanii wengi na vikundi vya hamasa vitakuwepo. Utakuwa ni mkesha wakipekee sana na kuacha kumbukumbu nyingi muhimu na kuwafanya wanadodoma kupata mtoko wa kiwilaya” alisema Alhaj Shekimweri.