Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa atoa siku 14 kwa Wakala wa Barabara (TANROADS), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) kuhakikisha mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga barabara ya Ibanda – Kajunjumele – Kiwira/Itungi Port (km 32) analeta vifaa na watalaam wote wanaohitajika eneo la mradi kwa mujibu wa mkataba.
Mradi wa barabara hiyo unafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 38 ambapo unatekelezwa na mkandarasi kutoka kampuni ya M/s AVM-Dillingham Construction International na kusimamiwa na Kitengo cha TECU kutoka Wakala wa Barabara(TANROADS).
Bashungwa ametoa agizo hilo Oktoba 2, 2023 wilayani Kyela mkoani Mbeya mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo ipo nyuma ya muda wa mkataba kwa asilimia 25 na kubaini mradi huo una upungufu wa watalaam na vifaa muhimu vinavyohitajika eneo la mradi.
“Naiagiza TANROADS, CRB na ERB kunipa taarifa ndani ya siku hizo na kama mkandarasi akishindwa kutekeleza kama mkataba unavyosema na tutalazimika kuchukua hatua ngumu basi tuzichukue haraka iwezekanavyo”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekwishatoa fedha kiasi cha Bilioni 3.7 kama sehemu ya malipo ya kwanza ya awali ya ujenzi huo na hadi sasa mkandarasi amekwishafanya maandalizi kwa asilimia 15 tu ukilinganisha na mahitaji ya mkataba.
“Kama unataka kujua rangi ya Mheshimiwa Rais chezea hii hela aliyoitoa Dkt. Samia… Mkandarasi umepewa hela ndo unaenda kufanya manunuzi ya vifaa Uturuki wakati ulitakiwa uwe navyo tayari na kuvileta eneo la mradi kipindi cha maandalizi”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa anafahamu mkandarasi huyo amepewa tena ujenzi wa barabara ya Sengerema – Nyehunge (km 54.4) ambapo ametilia shaka kasi ya mkandarasi huyo ambayo anaenda nayo kama ataweza kutekeleza mradi huo.
“Kama kilometa 32 zinakutoa jasho kweli utaweza kutekeleza zile kilometa 54 naomba TANROADS na CRB mumtizame kwa karibu mkandarasi huyu”, amesisitiza Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais ameridhia ujenzi wa barabara ya Isongole-Ipyana-Kasumulu-KatumbaSongwe (km 114.3) kwa kiwango cha lami kwa kuwa barabara hiyo ni muhimu na inaunganisha Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na Ileje iliyopo mkoani Songwe na hivi karibuni mkataba wake wa ujenzi utatiwa saini.
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa mtitiriko wa fedha kwenye shughuli za miradi ya maendeleo uko vizuri hapa nchini kinachohitajika ni sisi wenyewe kupanga vizuri vipaumbele vyetu.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, amesema kuwa mradi huo ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani humo kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri kutoka Kitengo cha TECU, Eng. Joel Mwambungu, ameeleza kuwa mkataba wa ujenzi na mkandarasi huyo ulisainiwa tarehe 27 Disemba 2022 na alitakiwa kuanza kazi tarehe 30 Machi 2023 mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Machi 2025.
Ameongeza kuwa hadi sasa mkandarasi amefanya maandalizi kwa asilimia 15 tu ukilinganisha na mahitaji ya mkataba na kazi zinazoendelea ni kusafisha eneo la ujenzi ambapo ameshamaliza kilometa 5.
“TANROADS imechukua juhudi za ziada kumsimamia mkandarasi ili alete mitambo eneo la kazi lakini mpaka sasa ni asilimia 15 ya kazi iliyofanyika na mitambo iliyoletwa haitoshi kuanza kazi ya ujenzi”, amefafanua Eng. Joel.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Ibanda – Kajunjumele – Kiwira/Itungi Port (km 32) ni muhimu kwa kuwa inaunganisha mji wa Kyela na Bandari ya Itungi na Kiwira pamoja na nchi jirani ya Malawi kupitia mpaka wa Kasumulu ambako kuna kituo cha Forodha.