Na Mwandishi wetu, Geita
WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde, ametembelea banda la kampuni ya Franone Mining and Gems LTD inayochimba madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, lililopo mjini Geita kwa kuwataka wachimbaji wadogo nchini wasijione wanyonge ila wachangamkie fursa za uchimbaji.
Waziri Mavunde amesema Serikali imeweka mazingira mazuri na mikakati bora kabisa katika kuwainua wachimbaji nchini.
Amesema baada ya mpango wa Building a Better Tomorrow (BBT) kufanikiwa katika Wizara ya Kilimo wapo mbioni kuanzisha mpango wa uchimbaji kwa maisha bora ya baadaye, Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) kwenye Wizara ya Madini.
“Wachimbaji wadogo msiwe wanyonge, tuna mpango wa kuwawezesha ili uchimbaji wenu uwe na tija kupitia dira ya 2030 madini ni maisha na utajiri,” amesema Waziri Mavunde.
Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya Franone Mining LTD, Napokye Baraka Kanunga amemuonyesha Waziri Mavunde madini ya Tanzanite na kusema yana rangi ya mvuto wa blue na yanabadilika rangi pindi ukiyashika na kuyageuza.
“Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD ndiyo inayomiliki machimbo ya madini ya Tanzanite kwenye kitalu C mji mdogo wa Mirerani na tumekuja kushiriki maonyesho haya ili kuwaonyesha wakazi wa kanda ya ziwa madini ya Tanzanite,” amesema Napokye.
Mchimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani, Fatuma Kikuyu amemueleza Waziri Mavunde, kuwawezesha wachimbaji wadogo ili wawe makampuni makubwa kama ya GGM LTD ya dhahabu na Franone Mining LTD ya Tanzanite.
Kikuyu amesema wachimbaji wadogo wanapaswa kupatiwa ruzuku ili waweze kupiga hatua na kuwa kama makampuni makubwa ya GGM Ltd ya dhahabu na Franone Mining Ltd ya Tanzanite.
“Wachimbaji wadogo tunafanya kazi kwenye mazingira magumu mno, hatukopesheki kwenye mabenki, tujengewe uwezo nasi tuwe kama GGM Ltd ya dhahabu na Franone Mining Ltd ya Tanzanite,” amesema Kikuyu.
Amesema gharama za uchimbaji kwa wachimbaji wadogo ni kubwa kwani zana za milipuko ni ghali, madeni, ankara za nishati ni kubwa, kwa hiyo wanafanya kazi katika mazingira magumu mno.
Hata hivyo, ameipongeza kampuni ya Franone Mining Ltd, kwa namna wanavyotoa ajira hasa kwa wanawake na kutengeneza miundombinu ya barabara inayopanda migodini.
Maonyesho hayo ya sita kimataifa ya teknolojia ya madini yamefanyika kwa muda wa siku saba kwenye kituo cha uwekezaji cha EPZA Bombambili mjini Geita na kuhusisha wa zaidi ya 5,000 kutoka taasisi na 300 kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Kenya, Malawi, Zambia, DRC Congo, Uganda, Rwanda, na Burundi.