Na Zillipa Joseph, Katavi.
Waganga wa tiba asili katika Halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoani Katavi wameshiriki katika kuishawishi jamii kupeleka watoto wenye dalili za ugonjwa wa surua kupata huduma katika vituo vya afya badala ya kutegemea tiba asili pekee.
Hali hiyo inafuatia juhudi zilizofanywa na Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaj Majid Mwanga ambaye aliwakusanya waganga hao wa tiba asili na kupatiwa elimu juu ya ugonjwa wa surua ambao ulilipuka mwishoni mwa mwaka jana na kusababisha vifo vya watoto 17 wa chini ya umri wa miaka nane.
Mlipuko wa ugonjwa wa surua ulianza mwezi Novemba mwaka 2022 hadi Machi 2023 katika halmashauri ya Mpimbwe ambayo imetajwa kuathirika zaidi na ugonjwa huo na baadae kuenea mkoa mzima wa Katavi; ambapo watoto wa umri wa miaka sifuri hadi nane walishambuliwa zaidi na uginjwa huo.
Zaidi ya watoto 4,000 wametajwa kuambukizwa ugonjwa huo unaoambukiza huku wazazi na walezi wao wakitegemea zaidi tiba asili kutoka kwa waganga wa jadi.
‘Nilimwogesha na kumpaka mtoto wangu na juisi ya ukwaju na pia nilimnywesha juisi hiyo lakini baada ya muda watoto wote wanne waliugua na nilimpoteza mdogo aliyekuwa na umri wa miezi saba’ alisema Sylivia Kimwela mkazi wa Maji Moto.
Mama huyo aliyekuwa na watoto wanne amesema tiba hiyo alielekezwa na majirani zake ambao nao walikuwa wakitumia kwa familia zao.
Bwana Juma Katani ni mmoja waganga wa tiba asili katika Halmashauri ya Mpimbwe, anakiri kuwa dawa za surua ziko nyingi na zimekuwa zikileta nafuu kwa wagonjwa.
Baadhi ya dawa alizodai kusaidia kutibu surua ni pamoja na juisi ya ukwaju, majani ya mlenda na mizizi ya mshona nguo.
‘Vitu hivyo vikichanganywa na dawa zingine mgonjwa anapona. Nimepokea wagonjwa wengi wa surua lakini surua ya kipindi hiki ilikuwa kali sana na tumepoteza watoto wetu’ alisema Juma.
Hata hivyo mganga huyo alisema elimu waliyopewa juu ya surua katika mkutano na mkuu wa wilaya ambapo waliazimia kuwashawishi wagonjwa kwenda hospitali imesaidia na wao kuokoa maisha ya familia nyingi.
Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaj Majid Mwanga alisema kutokana na mazingira ambayo watu wamekuwa wakiishi haikuwa rahisi kuwashawishi waganga hao wa tiba asili.
‘Kwanza waliniona kama adui ninayewanyang’anya wateja wao, lakini hali ilikuwa mbaya. Nilifanya operesheni maalum ya kuwapitia na kuzungumza nao hatimae walikubali kuja kwenye mkutano’ alisema Majid.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika chanjo ya surua Mratibu wa chanjo mkoa wa Katavi bwana Stephen Kahindi alisema wamefanikiwa kuchanja zaidi ya watoto laki mbili kwa mkoa mzima.
Aliongeza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa surua ulisababishwa na kukosekana kwa chanjo hiyo kwa miaka mitatu nyuma baada ya mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19.
Akieleza hali ya ugonjwa ilivyo kwa sasa Kahindi amesema wagonjwa wamepungua wodini ambapo mgonjwa mmoja hadi watatu wanaripotiwa kufika hospitalini ndani ya mwezi mmoja.
‘Kiukweli ugonjwa huu ulituendesha, ulikuwa ukifika kule Maji Moto kila familia ina mgonjwa’ alisema
Hata hivyo ameongeza kuwa kampeni ya chanjo ya nyumba kwa nyumba imesadia na anaamini hakutatokea mlipuko mwingine hivi karibuni na kuwasisitiza wazazi kujenga mazoea ya kukamilisha chanjo za watoto.