Na Victor Masangu,Kibaha
Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka katika kukiimarisha chama ameungana na wanachama wa chama cha mapinduzi (CCM) kata ya Kibaha kwa ajili ya utekelezaji wa ilani kwa vitendo amechangia kiasi cha shilingi milioni sita kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya chama.
Katika halfa hiyo ya harambee ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali,madiwani,wananchi pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya Jimbo la Kibaha mjini na vitongoji vyake vya jirani ikiwemo mlandizi.
Katika halfa hiyo Mbunge Koka amesema kwamba lengo lake na mikakati ambayo amejiwekea ni kukiimarisha chama cha mapinduzi katika kujenga ofisi za chama katika kata mbali mbali kwa lengo la kuweza kusaidia ufanisi wa kutekeleza majukumu ya chama ipasavyo.
Koka alisema kwamba endapo viongozi wa chama katika ngazi ya kata wakiwa na ofisi yao ya kudumu kutaweza kuwa ni chachu na mkombozi mkubwa kwa viongozi kutekeleza ilani kwa weledi mkubwa pamoja na wanachama wake kupata sehemu ya kwenda kusemea changamoto zao ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi wa haraka kwa ajili ya maendeleo.
“Leo nimefika hapa katika kata ya Kibaha lakini kitu cha Kwanza nafarijika sana wananchi wenzangu kuungana na mimi katika halfa hii ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya chama cha mapinduzi CCM kata ya Kibaha na mimi nimechangia milioni sita ambazo zitasaidia katika kumslizia ujenzi ikiwemo kuezeka paa kabisa katika ofisi hii,”alisema Mhe.Koka.
Pia katika halfa hiyo Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini mwalimu Mwajuma Nyamka naye aliunga juhudi za ujenzi huo kwa kuchangia kiasi cha shilingi laki tatu ambazo zitatumika katika kuiwekea ofisi hiyo tailizi za kisasa.
Naye Mwenyekiti wa UWT kata ya picha ya ndege Grace Junguru alisema anachangia kiasi cha shilingi milioni moja kwa lengo la kukiimarisha chama katika kuboresha miundombinu ya majengo lengo ikiwa ni kuweka mazingira. rafiki kwa viongozi wa chama.
Nao madiwani wa Halmashauri ya Kibaha wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wao Focusi Bundala pamoja na diwani wa viti maalimu Lidya Mgaya hawakuwa nyuma katika kuchagiza maendeleo walichangia kiasi cha shilingi laki saba ili kukamilisha mradi wa ujenzi huo.
Pia wadau mbali mbali wa maendeleo wakiwemo viongozi na wanachama wa CCM ambao walifika kumpa sapoti Mbunge Koka walichangia michango mbali mbali ya fedha,vifaa vya ujenzi,rangi,ambavyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa ofisi hiyo ambapo fedha zilizokusanywa pamoja na ahadi zote zimekusanywa zaidi ya milioni 11