Na Victor Masangu,Kibaha
Katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya michezo mke wa Mbunge la Jimbo la Kibaha mjini Selina Koka ameanzisha rasmi mashindano ya mchezo wa netiboli kwa wanawake wa jumuiya ya umoja wanawake (UWT) kata ya Misugusugu.
Mama Koka amezindua michuano hiyo ikiwa ni moja ya ahadi yake kubwa ambayo aliitoa ya kukuza na kuinua vipaji vya mchezo huo kwa wanawake wa kata zote 14 zilizopo katika Jimbo la Kibaha mjini ili kuweza kupata fursa ya wanawake kushiriki kikamilifu katika kukuza vipaji vyao.
Alibainisha kwamba hivi karibuni aliweza kufanya ziara yake katika kata mbali mbali akiwa Kama mlezi wa UWT Kibaha mji na alitoa na kukabidhi vifaa mbali mbali kwa timu husika ikiwemo mipira pamoja na jezi lengo ikiwa ni kila kata kuweza kuunda timu yao ya netiboli.
“Kwa kweli nimefarijika sana leo kuwepo hapa katika kata ya Misugusugu ikiwa nimekuja kuonana na wanawake wenzangu sambamba na kuzindua mashandano haya ambayo tumeyapa jina la Selina Cup na mm lengo langu ni kukuza vipaji zaidi katika mchezo huu wa netiboli,”alisema Mama Koka.
Kadhalika aliwahimiza wanawake wote wa UWT kuwa na mshikamano katika kushiriki katika mambo mbali mbali ikiwemo suala zima la michezo pamoja na kukiimarisha chama Cha mapinduzi kuanzia ngazi za chini kabisa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mji Elina Mgonja alimpongeza Mke wa Mbunge kwa ushirikiano wake wa kujitolea na kuwa karibu na jamii katika nyanja mbali mbali ikiwemo sekta ya michezo hususan netiboli kwa wanawake.
Hivi karibuni Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mji alipokuwa katika ziara ya Mwenyekiti wa UWT Kibaha mji aligawa vifaa mbali mbali vya mchezo wa netiboli katika kata 14 kwa lengo la kukuza na kuinua na kukuza vipaji vya wanawake wa Jimbo la Kibaha mjini.