Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dkt. Omar Dadi Shajak akizungumza wakati wa ziara ya kukagua Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Wilaya ya Mpwapwa, Dodoma leo Oktoba 01, 2023.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dkt. Omar Dadi Shajak akikagua mradi wa mbogamboga alipotembelea kitalu nyumba katika Kijiji cha Ng’hambi wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) wilayani Mpwapwa, Dodoma leo Oktoba 01, 2023.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dkt. Omar Dadi Shajak (wa pili kulia) akisikiliza maelezo kuhusu mradi wa kisima kirefu cha maji kilichojengwa katika Kijiji cha Kiegea kutoka kwa Mratibu wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) Wilaya ya Mpwapwa Bw. Aziz Bilu wakati wa ziara ya kukagua mradi huo leo Mpwapwa, Dodoma Oktoba 01, 2023. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Bi. Farhat Ali Mbarouk
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dkt. Omar Dadi Shajak akikagua ujenzi wa kituo cha huduma za mifugo katika Kijiji cha Ng’hambi wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) Mpwapwa, Dodoma leo Oktoba 01, 2023.
………………………….
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dkt. Omar Dadi Shajak amefanya ziara ya kukagua Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma leo Oktoba 01, 2023.
Amekagua miradi ya kisima kirefu na kitalu nyumba katika Kijiji cha Ng’hambi, mashine ya kukamua mafuta ya alizeti, ujenzi wa kituo cha huduma za mifugo na lambo katika Kijiji cha Ng’hambi na ujenzi wa kisima na josho la kuogeshea mifugo katika Kijiji cha Kazania yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara hiyo, Dkt. Shajak ameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuratibu vyema mradi huo unaotekelezwa katika pande zote mbili za Muungano.
Amesema mradi huo umeleta manufaa makubwa kwa wananchi kwa kuwasaidia kupata huduma za kijamii zikiwemo maji ambayo yamewawezesha kufanya shughuli za kujipatia kipato kama vile kilimo na ufugaji.
“Lengo la ziara hii ni kuangalia hatua zilizofikwa katiia utekelezaji wa Mradi wa EBARR kwa upande wa Bara lakini pia kujifunza namna gani mnaitekeleza ili na sisi kule Zanzibar tukaboreshe ili kufikia lengo la Serikali la kuwasaidia wananchi kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Pia, Katibu Mkuu Dkt. Shajak amewapongeza wasimamizi wa mradi huo wilayani Mpwapwa kwa kuisimamia kwa ufanisi kuanzia hatua ya ujenzi wake hadi kukamilika.
Amesema lengo la Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha inawasaidia wananchi wake waweze kuwa na Maisha mazuri licha kuwepo kwa changamoto za mazingira.
Hivyo amewahimiza wananchi waitumie miradi hiyo kujipatia huduma za kijamii hususan maji kutokana na visima na malambo yanayojengwa katika maeneo yao kupitia miradi hiyo ya mazingira.
Kwa upande wao wanakijiji wa vijiji vilivyotembelewa na Katibu Mkuu kupitia kwa Diwani wa Kata ya Nghambi Richard Milimo wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradio wa EBARR na kuwema kuwa ni mkombozi kwao.
Wamesema kwa muda mrefu walikuwa wakihangaika kutafuta maji umbali mrefu hali iliyochangia uchumi kushuka na sasa hivi baada ya kuchimbiwa visima wanaendesha maisha yao vizuri.
“Tumeupokea mradi huu vizuri na sasa hivi tunalima mbogamboga na nyanya katika kikundi chetu na tunauza mazao yetu na kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha, tunaomba mumfikishie salamu na shukrani hizi Rais wetu na Makamu wake,” wamesema wananchi wa vijiji hivyo.
Katibu Mkuu Dkt. Shajak katika ziara hiyo aliambatana na Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Bi. Farhat Ali Mbarouk pamoja na Mratibu wa Mradi wa EBARR Wilaya kaskazini ‘A‘ Bw. Alawi Haji Hija.
Mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) unatekelezwa katika wilaya za Mpwapwa (Dodoma), Simanjiro (Manyara), Mvomero (Morogoro) na Kishapu (Shinyanga) kwa upande wa Bara na Kaskazini-A (Unguja) kwa upande wa Zanzibar.