Name Ashrack Miraji
Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni amesisitiza wakazi wa wilaya hiyo kuedelea kujitolea kwenye shughuli mbalimbali ikiwemo kuibua miradi ya maendeleo na ile ya kuboresha huduma katika maeneo yao, miongoni mwa hatua muhimu ya kuunga mkono juhudi na serikali katika kuboresha huduma.
Ameyasema hayo wakati wa mwendelezo wa ziara zake kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi ambapo mara hii alikua katika kata za Vuje na Bombo pia kushiriki Msaragambo kwenye ujenzi wa shule ya Sekondari Vuje inayojengwa kwa nguvu za wananchi.
Akiwa katika kata ya Vuje amekagua mradi wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita Nane inayogharimu kiasi cha shilingi Milioni 298, Mradi wa Maji unaotekelezwa na RUWASA ambao mpaka kukamilika kwake umepangwa kugharimu shilingi Bilioni 1.52.ambako ameeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wake.
Akiwa katika kata ya Bombo alitembelea mradi mkubwa wa Maji unaogharimu zaidi ya shilingi Milioni 600 mradi unaotekelezwa na RUWASA ambapo amemtaka mkandarasi kuongeza kasi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakatiili kuondoa uhaba wa Maji katika eneo hilo.
“Niendelee kumshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kuendelea kutujali sisi wakazi wa Same kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, ahadi yetu na mimi nikiwa msimamizi mkuu wa shughuli za serikali kwenye wilaya hii ya Same ni kusimamia kwa karibu fedha zote tunazopewa kuhakikisha zinatumika kama ilivyo elekezwa”.Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Ametembelea pia Shule ya bweni ya Bombo na kuzungumza na wanafunzi wa Shule hiyo akiwatahadharisha dhidi ya masuala ya mmomonyoko wa maadili ikiwemo tabia ya baadhi ya watu kueneza mchezo mchafu kushiriki mapenzi wa Jinsia Moja (ushoga na usagaji) na kuwataka wanafunzi hao kutumia muda wao vizuri kwa kuzingatia masomo waweze kupata fursa ya kuwa viongozi na wazazi wema katika jamii.