Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akifungua Mkutano wa 52 wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya jijini Dar e Salaam Septemba 30, 2023.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiteta jambo na Ameer na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania Shekh Tahir Mahmood Choudhry wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 52 wa Jumuiya hiyo jijini Dar e Salaam Septemba 30, 2023.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis alikabidhiwa msahafu na vitabu mbalimbali vinavyohusiana na hiyo Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya wakati wa Mkutano wa 52 wa jumuiya hiyo jijini Dar e Salaam Septemba 30, 2023.
………………………….
Taasisi za dini na viongozi wake wametakiwa kuchukua hatua stahiki katika kurekebisha mmomonyoko wa maadili unaotokana na utandawazi na matumizi yasiyofaa ya teknolojia.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akifungua Mkutano wa 52 wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya jijini Dar e Salaam Septemba 30, 2023
Amesema kuwa taasisi za dini zina jukumu la lililotukuka katika kujenga jamii bora ya watanzania akisisitiza kuwa hakuna ustawi thabiti wa jamii ikiwa haina maadili stahiki kuweza kuivalisha nchi haiba iliyotukuka kwa watu wenye uadilifu, heshima na mwisho wa yote kuipenda nchi yao.
“Viongozi wa dini hili ndilo jukumu lenu la msingi la kutulea waumini tuwe na tabia njema ili hatimae tuweze kuwa wapenzi au wateule wa Mungu. Nina imani kubwa kwamba mtu hawezi kuwa mpenzi wa Mungu kisha akaacha kutenda maadili mema kwa viumbe wengine hasa wanadamu wenzake,” amesema Mhe. Khamis.
Naibu Waziri Khamis amesema elimu kwa watoto ndilo jambo litalowajengea msingi imara wa kuwa raia wema na wa kutegemewa kuliongoza taifa la kesho kupitia mafunzo sahihi ya kimaadili ndipo kizazi chetu kitaepukana na mmomonyoko wa maadili.
Vilevile ameipongeza Jumuiya ya Waislam Waahmadiyya kwa kuonesha mfano mzuri wa upendo na kuvumiliana miongoni mwa waumini wa dini na itikadi zingine.
Amewapongeza kwa Sera ya kushughulikia masuala ya dini bila kuchanganya na siasa pamoja na kuwa kwenu watiifu kwa sheria za nchi na Serikali zilizopo madarakani kuwa inawajengea heshima.
Aidha, Mhe. Khamis amewapongeza kwa utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii kama vile elimu, afya na maji safi na salama kupitia uchimbaji wa visima vya maji katika maeneo kadhaa nchini ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo.
“Tunatambua kwamba ni wajibu wa Serikali kupeleka huduma hizi kwa wananchi wake ndio maana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejidhatiti katika kuhakikisha inajenga uwezo wa kutoa huduma hizi kwa ubora na viwango vinavyokubalika,” amesema.