Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (wa kwanza kulia) akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwenye Maonesho ya Teknolojia ya Madini yaliyofungwa leo mkoani Geita.
……………………….
Na. Judith Lema – GCLA
Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sabanitho Mtega, amewataka wadau wa kemikali hususani wachimbaji wadogo wa dhahabu kuzingatia matumizi salama ya kemikali kulingana na Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Na. 3 ya mwaka 2003 wakati wa uchenjuaji wa dhahabu.
Wito huo ameutoa leo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye maonesho ya sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.
“Sekta ya madini ni sekta moja wapo yenye matumizi makubwa sana ya kemikali hasa katika utafutaji na uchimbaji wa madini, hususani madini ya Dhahabu. Sisi kama Mdhibiti na Msimamizi wa Sheria ya Kemikali nchini, tunawajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba tasnia hii wanapata elimu ya matumizi salama ya kemikali, lakini pia wanafahamu madhara ya matumizi yasiyo salama ya kemikali na kitu gani wafanye pindi madhara ya matumizi yasiyo salama ya kemikali yanapotokea”. Amesema Mtega.
Mtega amesema kuwa kemikali zipo katika maeneo mengi lakini kinachokosekana ni ufahamu wa matumizi salama ya kemikali hususani kwa wachimbaji wadogo.
Kwa upande wake Meneja, Ofisi ya Kanda ya Ziwa, Musa Kuzumila, amesema kuwa Mamlaka kupitia maonesho haya imeweza kutoa elimu ya matumizi salama ya Zebaki kwa kundi la wachimbaji wadogo wanaohusika na uchenjuaji wa dhahabu katika maeneo ya mkoa wa Geita na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.
“Zebaki ni miongoni mwa kemikali hatarishi kwa afya na mazingira, hivyo kundi hili la wachimbaji wadogo ni vyema wakapata ufahamu wa jinsi ya kutumia kemikali hii ili kuepusha kupata athari ya afya zao na mazingira”. Alisema Kuzumila.
Hata hivyo, ametoa wito kwa waajiri wa wachimbaji wadogo kutengeneza mazingira mazuri ya kuwakinga wafanyakazi hao na madhara ya kemikali kwa kuwapatia vifaa kinga na elimu juu ya matumizi salama ya kemikali.
Naye, Musa Shunashu, Afisa Uhusiano kutoka kampuni ya Geita Gold Mine, ambaye ni mmoja wa Wadau wa Kemikali amesema kuwa katika maonesho haya ameweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na jinsi gani ya kutumia na kutunza kemikali aina ya Sodium Cyanide ambayo hutumika katika kuchenjua dhahabu kwenye migodi.
Kwa upande wake, Afisa Mawasiliano kutoka kampuni ya Waja General Chemicals, Simoni Masunga, ameishukuru Mamlaka kwa kuendelea kutoa elimu ya matumizi salama ya kemikali kwa wadau wanasafirisha Sodium Cyanide ambayo imewawezesha kuanza kutumia magari maalum aina yanayokidhi vigezo vya kusafirisha kemikali kwa usalama kwa ajili ya usalama wa watu na mazingira.