Tamasha la Ngoma za Asili lijulikanalo kama “ *Tulia Traditional Dances Festival* ” ni kichocheo kikubwa katika kukuza ajira na utalii nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ameyasema hayo wakati akihitimisha tamasha hilo lililoambatana na mbio za “Tulia Marathon” lililofanyika leo Septemba 30,2023 jijini Mbeya.
“Tamasha hili ni moja ya zao jipya la utalii wa utamaduni ambalo limekuwa ni chombo muhimu cha kukuza na kuhifadhi utamaduni wa Tanzania kupitia Ngoma za Asili” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Amefafanua kuwa tamasha hilo limekuwa na manufaa makubwa kwa jamii na wasanii wa Ngoma za Asili kwa kusaidia kukuza na kutambulisha tamaduni za Tanzania, kutoa ajira pamoja na kuchochea ukuaji wa utalii katika jiji hilo kwa kuwavutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesema Tamasha hilo ni mwendelezo wa jitihada za kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kuongeza mazao ya utalii.
Amewataka wadau na washiriki wa tamasha hilo kutumia fursa ya uwepo wa tamasha hilo kuwekeza katika shughuli mbalimbali za utalii kama vile wakala wa biashara za utalii, kujenga kambi za kulala wageni, kujenga hoteli, kumbi za mikutano na maeneo ya michezo mbalimbali mkoani Mbeya.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameiomba Serikali kuunga mkono tamasha hilo kwa lengo la kuhakikisha utalii unakua katika ukanda wa Nyanda za juu Kusini.
Tamasha la Ngoma za Asili lililoandaliwa na Taasisi ya Tulia Trust, lilianza tarehe 28 hadi 30 Septemba, 2023 lengo ikiwa ni kuenzi asili na utamaduni wa Mtanzania pamoja na kukuza zao jipya la Utalii wa Utamaduni hasa katika Nyanda za Juu Kusini.