Na Sophia Kingimali
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kuwa na utamaduni wa kuweka kumbukumbu zao kwa ajili ya maslahi yao na taifa kwa ujumla huku akitoa rai kuanzishwa kwa tovuti ya serikali itakayoweka kumukumbu za viongozi
Hayo ameyasema leo septemba 30 wakati akizindua tovuti ya kuhifadhi nyaraka za Dkt. Salim Ahmed Salim hafla iliyofanyika jijini Dar es salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Julius nyerere JNICC.
Amesema familia ya Dkt. Salim ndiyo waliokuja na wazo hilo la kuweka tovuti maalumu hivyo ni wakati sasa wa serikali kufikiria namna ya kuanzisha tovuti ya serikali kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za viongozi.
“Hili ni wazo la familia ambalo lililetwa kwetu kama serikali nikaona nijambo Zuri na nikaelekeza serikali kulisimamia lakini hili kwetu limetuamsha na kutukumbusha umuhimu wa kuhifadhi historia zetu”amesema Dkt Samia
Aidha amesema kuwa tovuti hiyo itaakisi safari ya maisha halisi ya Dkt.Salim Ahmed Salim lakini pia itatoa fursa ya kutambua historia ya nchi.
Amesema Dkt.Salim alifinya makubwa Afrika na Duniani kote ikiwemo kuanzisha baraza la usuluhishi pamoja na kuwa katibu mkuu wa kwanza kwenda Afrika Kusini na kupambana na ubaguzi wa rangi.
“Hizi ni hazina kwa taifa viongozi waliopo na watakaokuja wanapaswa kujifunza ikiwemo uvumilivu kama alivyo Dkt Salim”amesema
Sambamba na hayo Rais ameitaka taasisi ya uongozi kumsaidia Rais wa awamu ya nne kukamilisha kitabu chake na kukiweka kwenye tovuti.
Pia Rais Dkt Samia amesema chuo cha Diplomasia kwa sasa ni mali ya serikali na amekibadilisha jina na kukiita kituo cha diplomasia cha Dkt Salim Ahmed Salim.
Kwa upande wake waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora George Simbachawene akizungumza wakati akimkaribisha Rais amesema hii ni tovuti ya kwanza kwa kuhifadhi nyaraka za serikali.
Amesema wizara itaongeza bajeti kwa mwaka huu wa fedha ili kuongeza nguvu kwenye kuhifadhi wa kumbukumbu ikiwezekana kufungua tovuti ya serikali ambayo itatumika kuweka kumbukumbu za viongozi.
” Taasisi ya Uongozi ndio iliyosimamia upatikaji wa hii tovuti lakini pia walisimamia kitabu cha Rais wa awamu ya pili Dkt. Ally Hassan Mwinyi na kitabu cha Rais wa awamu ya tatu hayati Dkt Benjamini Mkapa sasa nafikiri huu ni wakati sahihi wa kuanza kuweka kumbukumbu za viongozi wakiwa hai ili historia zao ziweze kuwa funza kwa vijana ambao ndio viongozi wa kesho”amesema Simbachawene.
Nae,Balozi Christopher Lihundi amewataka vijana kutumia tovuti hiyo kama sehemu ya urithi wa Bara la Afrika ili kujifunza maswala mbalimbali ikiwemo uongozi.
Lakini pia balozi Lihundi amewataka wanasiasa kuiga uvumilivu kama akiokuwa nao dkt Salim Ahmed Salim
Kwa upande wake Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema mawazo ya Dkt. Salim yalizingatia zaidi utaifa hivyo ni wakati wa viongozi kujifunza kupitia maandiko yake mbambali yaliyoko kwenye tovuti
Nae,mtoto wa Dkt. Salim,Ahmed Salim ameishukuru serikali kwa kuwaunga mkono katika jitihada zao za kuandaa tovuti hiyo ambayo itatoa elimu ya namna ambayo aliishi Dkt Salim katika maisha ya uongozi.
Amesema tovuti hiyo itakua endelevu na itapatikana bila gharama lengo ni kila mtu kujifunza na kuijua historia ya nchi.
Dkt. Salim Ahmed Salim alikua waziri mkuu wa tano na Katibu Mkuu wa 8 lakini pia alikuwa mwanadiplomasia mzuri na mwenye mchango mkubwa kwa taifa lakini sasa hivi ni mgonjwa ambapo leo ameshidwa kuhudhuria tukio hilo muhimu kwenye maisha yake hivyo amewakilishwa na familia yake.