Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde akimsikiliza Kaimu Meneja Mawasiliano na Masoko Wakala wa Majengo Tanzania TBA Fredrick Kalinga wakati alipotembelea banda la TBA kwenye maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kwenye viwanja vya EPZ Bombambili mjini Geita.
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde akitaka ufafanuzi kwa baadhi ya mambo kutoka kwa Kaimu Meneja Mawasiliano na Masoko Wakala wa Majengo Tanzania TBA Fredrick Kalinga wakati alipotembelea banda la TBA kwenye maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kwenye viwanja vya EPZ Bombambili mjini Geita.
…………………………….
Na John Bukuku, Geita
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amepongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kazi wanayoendelea kuifanya ambayo imeleta mapinduzi katika sekta ya ujenzi. Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Septemba 29,2023 baada ya kutembelea banda la TBA katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZA Bombambili, mkoani Geita. Amesema nyumba zinazojengwa na wakala huo kwa sasa zina ubora wa kisasa zikiwemo za zilizojengwa Masaki jijini Dar es Salaam.
“Nimeziona nyumba mlizojenga Masaki ni nzuri na mnazozijenga sasa mtu hawezi kujua kama zimejengwa na taasisi ya Serikali, mnakwenda sambamba na matakwa ya mahitaji ya soko,” amesema Mavunde.
Naye Kaimu Meneja Mawasiliano na Masoko TBA, Fredrick Kalinga, amesema anamshukuru Mhe. Rais kwa kuona haja ya kufanya mabadiliko ya sheria iliyoanzisha wakala huo kwa GN namba 595 ya Agosti 25, 2023 ambayo inawaruhusu TBA kushirikiana na Sekta binafsi katika kuendeleza miliki nchini ambapo nyumba watakazojenga kwa kushirikiana na Sekta binafsi zitapangishwa au kuuzwa kwa watu wote hata wasio watumishi wa umma tofauti na hapo awali walipohudumia watumishi wa umma pekee.
Amesema pia wanaendelea na miradi mingine mipya na kwamba wanatarajia kujenga nyumba katika mikoa mbalimbali ukiwemo Mkoa wa Geita. Wakala huo umejenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato, ofisi ya mkuu wa wilaya ya Nyang’wale na jengo la Tanesco Mkoa wa Geita pamoja na Wilaya cha Chato. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 TBA imetekeleza miradi 157 inayojumuisha 93 ya usimamizi na ushauri, 33 ya ujenzi, 15 ya buni jenga na miradi 16 ya fedha za ndani.