NA JOHN BUKUKU, GEITA
Wanawake nchini wametakiwa kutumia nishati mbadala katika kufanikisha shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia jambo ambalo litasaidia kuepuka uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo kuchoma mkaa, matumizi ya kuni hali ambayo inapelekea kuwepo kwa majanga ya asili yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Wakizungumza umuhimu wa kutumia nishati mbadala ikiwemo gesi kwa ajili ya kupikia wakati walipotembelea banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwenye Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kwenye Viwanja vya EPZ Bombambili Mkoani Geita, Wakazi wa Mkoa huo, wamesema kuwa wakati umefika wa kutumia nishati mbadala ili kutunza mazingira.
Mkazi wa Geita Bi. Upendo Francis, amesema kuwa amenunua gesi kwa ajili ya kupunguza gharama wakati wa kuandaa chakula kwani matumizi ya mkaa ni bei kubwa.
Amesema kuwa matumzi ya gesi ni muhimu kutokana yanasaidia kuandaa chakula kwa haraka na wakati sahihi.
“Gesi inatusaidia pia wakati wa asubuhi kuandaa chai mapema ili tuweze kuwahi katika shughuli za uchumi” amesema Bi. Francis.
Amesema kuwa matumizi ya gesi ni mazuri kutokana yanatuepusha na uharibifu wa mazingira pamoja na kukata miti kwa ajili ya kuni za kupikia.
Nae Felister Zakambo, amesema kuwa matumizi ya nishati mbadala inawasaidia kutunza mazingira kwa asilimia kubwa.
“Matumizi ya nishati mbadala yanakwenda kutunza vyanzo vya maji ikiwemo miti kwani awali asilimia kubwa tulikuwa tunatumia kuni au mkaa kwa ajili ya kupikia” amesema Bi. Zakambo.
Ametoa wito kwa wanawake wote nchini kutumia gesi katika shughuli za kibinadamu ikiwemo kupikia kwani ni rafiki na inaokoa muda pamoja na kutunza masufuria yasichafuke na kuharibika haraka.