Mwamvua Mwinyi, Mafia
SERIKALI imewasihi wadau na wawekezaji mbalimbali wakiwemo wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa anga na bahari ndani na nje ya Tanzania , kuwekeza kisiwa cha Mafia , Mkoani Pwani ili kuweka mazingira rafiki ya usafirishaji kwa watalii .
Aidha imewasihi wawekezaji kushirikiana na Serikali kufanya uwekezaji katika uvuvi,kilimo cha Mwani na ufugaji viumbe maji,majongoo bahari ili kuongeza thamani ya mazao ya bahari.
Akifunga kongamano la utalii na uwekezaji Mafia, Mkoani Pwani Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ,Agnes Kisaka Meena alieleza Mafia ni kivutio cha uwekezaji wa uchumi wa bluu na mazalia ya samaki Duniani hivyo Serikali itaendelea kutangaza vivutio vilivyopo ili iweze kujitangaza zaidi ulimwenguni.
“Serikali itaendelea kutangaza utalii,ili kuvutia wawekezaji na kuongeza watalii nchini na hili limetiwa nguvu kubwa na filamu ya royal tour iliyoongozwa na Rais wetu Samia Suluhu Hassan”na imani yetu wawekezaji mbalimbali na watalii wataendelea kuongezeka”
Agnes alieleza, kutokana na juhudi hizo pia Serikali imeanza mchakato kuwezesha wavuvi wadogowadogo katika kuwapatia mkopo nafuu, kufanya shughuli za uvuvi na viumbe maji,kilimo cha Mwani na ufugaji samaki kwenye vizimba ili kuinua kipato cha wananchi na wavuvi kupitia ukanda wa bahari.
Vilevile ,ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa Mkoani Lindi ambayo itachagiza na kuchechemua uwekezaji wa bahari kuu, viwanda vya kuchakata samaki.
Awali mkuu wa wilaya ya Mafia Zephania Sumaye alieleza , asilimia 70 ya mapato halmashauri ya Mafia inategemea utalii na uchumi wa bluu.
Alieleza, Mafia ni kivutio cha uwekezaji katika uchumi wa bluu, ikiwemo uvuvi endelevu, ufugaji wa viumbe maji, viumbe bahari,utalii na usafirishaji baharini.
Zephania alieleza,wanaendelea kuboresha miundombinu ya uwekezaji katika miundombinu mbalimbali, kuitangaza Mafia ambapo wamejipanga kutenga maeneo na kongani ili kuvutia wawekezaji.
Fidelis Obanga ambae ni Meneja Kanda ya Mashariki TIC aliwaomba wawekezaji kufuata sheria na utaratibu wa uwekezaji ili kuondokana na changamoto zinazojitokeza wakati wa mchakato wa uwekezaji.
Katika kongamano hilo Lilian Kapakala, Meneja wa Kanda ya Mashariki Kusini, Baraza la Taifa Uhifadhi wa Mazingira (NEMC ),alitoa rai kutunza mazingira kwa mujibu wa sheria na kuwa na uchumi wa bluu unaoendana na utunzaji wa mazingira.
Lilian alitahadharisha wilaya hiyo kuimarisha utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya baadae.
Kwa upande wake Moez Kassam, Mwekezaji Mafia anasema ataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua sekta ya uwekezaji ili kuongeza uchumi na pato la Mafia.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2023/09/IMG20230929131448-1024x768.jpg)
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2023/09/IMG20230929124321-1024x768.jpg)
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2023/09/IMG20230929115817-1024x768.jpg)