Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile (mwenye shati ya mikobo mifupi) akiwasikiliza wataalam kuhusu shughuli zinazofanywa kituo cha kuratibu shughuli za Utafutaji na Uokoaji (MRCC), wakati alipotembelea kituo hicho kinachoendeshwa na Shirika la Uwakala wa Meli Nchini (TASAC), Jijini Dar es Salaam.
…..
Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile amelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa usimamizi na udhibiti vyombo vya usafiri majini nchini hali inayochangia ongezeko la uwekezaji wa usafiri huo nchini.
Akizungumza wakati alipotembelea Ofisi za Shirika hilo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. Kahenzile amesema Uwekezaji unaofanywa na Serikali na sekta binafsi katika usafiri huo unahitaji ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha abiria na mizigo inasafirishwa kwa kuzingatia usalama.
“Serikali inaendelea na maboresho ya miundombinu ya bandari lakini pia inatekeleza miradi ya ujenzi wa meli katika maziwa yetu lakini pia sekta binafsi imeendelea kuwekeza kwa kununua meli nyingi za kisasa hususani kwenye bahari na kutoa huduma za usafirishaji hivyo kwa kasi hiyo utaona hayo ni miongoni mwa matokeo ya kazi nzuri mnayoifanya’ amesema Naibu Waziri Kihenzile.
Naibu Waziri Kihenzile amesema katika kuimarisha usalama kupitia utafutaji, uokoaji na utoaji wa taarifa za mbalimbali za usafiri majini tayari Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi kujenga kituo cha Utafutaji na Uokoaji katika Ziwa Viktoria.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Nelson Mlali amesema shirika limeendelea kupata mafanikio ikiwemo ongezeko la utoaji wa leseni na vyeti vya usajili ambapo kwa 2020/22 vyeti 1,278 vilivtolewa ukilinganisha na vyeti 941 kwa mwaka 2018/19.
Mlali ameongeza kuwa TASAC imefanikiwa kupata hati safi za ukaguzi wa Hesabu kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2018/19 na 2020/21.Naye Afisa wa TASAC kutoka kituo cha kuratibu Shughuli za utafutaji na Uokoaji (MRCC) Emmanuel Lusuva amesema taarifa mbalimbali muhimu za majini zimekuwa zikitolewa kwa wadau mara tu zinapojitokeza hali inayosababisha kuimarishwa kwa sekta ndogo hiyo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile yuko jijini Dar es Salaam kwa ziara ya siku 6 ya kukutana na menejimenti za taasisi za Wizara na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na taasisi hizo.