Na. WAF – Washington USA.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeingia makubaliano na Serikali ya Marekani juu ya uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa masuala ya Afya kwa kwa kuanzisha Maabara za Taifa za Afya ya Jamii za kisasa.
Makubaliano hayo yamefikiwa mara baada ya Waziri wa Afya Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui kufanya kikao na Mkuu wa Masuala ya Kimaita Idara ya Afya na Huduma za Kibinadamu nchini Marekani Bi Susan Kim, kwa kujadiliana kuhusu uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa masuala ya Afya.
“Tumekuja hapa kujifunza jinsi idara hiyo inavyosimamia na kuratibu huduma za maabara za Kitaifa za Afya ya Jamii ambapo tumekubaliana kuanzisha Maabara za Taifa za Afya ya Jamii ambazo zitakuwa na jukumu la ufuatiliaji wa magonjwa hususani yanayoathiri afya ya jamii na vihatarishi vyake, uchunguzi wa magonjwa na tafiti za masuala ya afya ya jamii” amesema Waziri Ummy Mwalimu
Amesema, uanzishwaji wa maabara hizo utaimarisha uwezo wa Tanzania katika kujikinga, kujiandaa na kukabiliana na majanga ya afya kama vile UVIKO 19, Marburg na Ebola.