Na Eleuteri Mangi, Cairo Misri
Nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zimepata dhamana ya kuandaa Mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027).
Akiongea mara baada ya kutangazwa matokeo hayo na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Dkt. Patrice Motsepe, Waziri wa Utamaduni, Sanaa Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema mpambano ulikuwa mkubwa na hatimaye EA Pamoja Bid ndiyo iliyopewa dhamana ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
“Tunawashukuru viongozi wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Dkt. William Ruto wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda kwa utayari wao na kuunga mkono jambo hili kwa pamoja, hii imekuwa alama muhimu kwetu kuwa nchi zetu zipo tayari kuwa mwenyeji wa AFCON 2027” amesema Dkt. Ndumbaro.
Mashindano hayo kufanyika nchi za Afrika Mashariki ni dhamana kubwa kwa kuwa ni mara ya kwanza mashindano hayo kufanyika katika nchi hizo tangu mashindano hayo kuanzishwa miaka 66 iliyopita ikiwa ni mwaka 1957.
Mawaziri wa Michezo wa nchi hizo, Mhe. Dkt. Damasi Ndumbaro, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Tanzania, Mhe. Ababu Namwamba, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Kenya na Mhe. Peter Ogwang, Waziri wa Nchi Elimu na Michezo, Uganda wamekuwa mstari wa mbele Cairo nchini Misri kufanikisha suala hilo.
Nchi ambazo zilikuwa kwenye kinyang’anyiro hicho ni Tanzania, Kenya na Uganda kwa kauli ya EA Pamoja Bid, Algeria, Benin na Nigeria, Botswana pamoja na Senegal.