Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhe. Mayeka Simon Mayeka amelipongeza Shirika la Madini la Taifa STAMICO kwa uamuzi wake wa kushirikiana na vikundi mbalimbali katika uchimbaji.
Hayo ameyasema alipotembelea banda la STAMICO wakati wa maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kwenye viwanja vya EPZ Bombambili mjini Geita.
Amesema STAMICO imefanya jambo la kishujaa la kuwakumbuka watu wa makundi maalumu ambayo yamekuwa yakisahaulika katika shughuli za kiuchumi.
Ameipongeza tena kwa kushiriki kikamilifu katika suala nzima la kutunza mazingira kwa kuzalisha mkaa mbadala sambamba na kupanda miti katika maeneo mbalimbali.
Ameitaka STAMICO kuendelea kutoa elimu ya matumizi mbadala ya magogo (Matimba) ambayo ni chuma katika shughuli za uchimbaji.
“Niwapongeze STAMICO kwa jitihada mnazozifanya za kuwaendeleza wachimbaji wadogo, naomba mzidi kutoa elimu ya matumizi mbadala wa miti katika uchimbaji ili kupunguza ukataji wa miti” alisisitiza Mhe. Mayeka Simon Mayeka.