Na Sophia Kingimali
Shirikia la Umeme Tanzania (TANESCO)limesema kuwa uwepo wa mgawo wa umeme umetokana na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa maji katika vyanzo vya kuzalishia umeme lakini pia ongezeko la shughuli za kiuchumi.
Haya yamebainishwa leo Septemba 27 na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Gissim Nyamo-Hanga alipokua akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme nchini.
Amesema upungufu huo umetokana pia na upungufu wa maji kwenye vituo vya kufua umeme ambapo yametokana na mabadiliko ya tabia nchi lakini pia matengenezo yanayoendelea kwenye visima vya gesi asilia na mitambo ya kuzalisha umeme wa gesi asilia.
“Baadhi ya maeneo nchini yamekua yanakosa huduma ya umeme kwa nyakati tofauti kutokana na sababu hizo lakini matarajio yetu ni kuhakikisha swala hili linaisha kwa wakati”amesema Nyamo-Hanga.
Asemema shirika limeanza kutekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuharakisha matengenezo ya mitambo hiyo ili kuwaondolea wananchi changamoto inayowakabili kwa sasa.
“Ni matarajio yetu mwezi oktoba tutakamilisha matengenezo hayo ambayo yatawezesha kupata nafuu ya makali ya upungufu ya upungufu wa umeme na ndani ya miezi sita tutahakikisha tunaondokana na kadhia hii”amesema.
Aidha ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius nyerere kutasaidia kuondoa tatizo la umeme nchini.
Amesema mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawatt 2115 ambapo kwa sasa shirika linauwezo wa kuzalisha megawatt 1900.
“Mradi wa Julius Nyerere mpaka sasa umefikia asilimia 92 pindi mradi ukikamilika na kuingizwa kwenye gridi ya taifa utachangia kuimarika kwa hali ya umeme nchini”ameongeza
Aidha shirika limewataka wananchi kuwa na uvumilivu kwa kipindi hiki ambacho wanakabiliwa na changamoto huku akitoa rai kwa wananchi kupanda na kutunza miti ili kusaidia utunzaji wa mazingira.