Na WMJJWM Dar Es Salaam
Jamii imehamasishwa kushiriki katika Tamasha la Maendeleo la kutangaza Fursa za Kouchumi na kupinga Ukatili (ZIFIUKUKI) lenye lengo la kuileta Jamii sehemu moja kupata elimu na huduma mbalimbali za kijamii.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa rai hiyo wakati akizungumza na waandishi wa Habari Septemba 25, 2023 jijini Dar Es Salaam.
Waziri Dkt. Gwajima amesema jukumu la kuzuia vitendo vya ukatili ni la kila mwanajamii na kila taasisi hivyo Wizara inashirikiana na Wadau mbalimbali kuelimisha jamii kupinga ukatili na kufikia fursa za kiuchumi ili kutokomeza umaskini ambapo pia huchochea ukatili.
Aidha ameiomba Ofisi ya Rais- TAMISEMI kupitia viongozi wa mikoa husika kulipokea Tamasha hili na kuwaelekeza Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kushiriki kuratibu Matamasha hayo katika Mikoa na Halmashauri.
“Nawaomba Wadau mbalimbali wanaofanya kazi na Wizara kushirikiana kubeba ajenda ya kuhamasisha, kutoa huduma na kuelimisha jamii ifahamu na kutambua fursa mbalimbali za kiuchumi kupitia Tanzania Development Festival Kampeni ya ‘ZIFIUKUKI’ alisema Waziri Dkt Gwajima
Pia ametoa wito kwa Wadau wote kujitokeza kwa wingi kushiriki katika jukwaa hilo la pamoja ili kuelimisha wananchi juu ya fursa za kiuchumi na kupata huduma nyingine mbalimbali za kijamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la FAGID linaloandaa tamasha hilo kwa kushirikiana na Wizara, Simon Mwapagata amesema Shirika hilo limeamua kuibeba ajenda ya kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwa lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo wasanii kwa lengo la kutoa elimu hasa Vijijini na kuwaunganisha na fursa za kiuchumi katika maeneo yao.
Tamasha la Zijue Fursa Imarisha Uchumi Kataa Ukatili Kazi Iendelee ni Kampeni Shirikishi ya Serikali na Wadau wa FAGDI ambao ni muunganiko wa wasanii mbalimbali. Lengo la Kampeni ya ZIFIUKUKI ni kutoa elimu kwa jamii hasa kuzifahamu na kuzifikia fursa za maendeleo na kujiimarisha kiuchumi ili kupambana na vitendo vya ukatili.