NA SHEHA HAJI & IBRAHIM DUNIA- HABARI MAELEZO- 25/09/2023
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imeweka mazingira rafiki kwa wananchi ili kujikwamua kiuchumi.
Ameyasema hayo katika Ufunguzi wa Tamasha la Fahari ya Zanzibar lililoandaliwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi kiuchumi Zanzibar (ZEEA) lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip huko Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Rais Mwinyi amesema Serikali Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi zinazochukuliwa na wananchi za kujiajiri wenyewe hivyo itahakikisha inaweka miundombinu rafiki itakayowawezesha kuzitumia vyema fursa za ujasiriamali zilizopo ikiwemo uwepo wa hoteli mbali mbali nchini.
Aidha, amewasisitiza wajasiriamali kuzalisha bidhaa zinazoendana na soko ili kuinua kipato chao pamoja na kuzitaka taasisi mbali mbali kubuni na kuzitumia vyema fursa za kibiashara ili wananchi waendelee kufaidika zaidi.
Rais Mwinyi ametoa wito kwa wajasiriamali waliopatiwa mikopo nafuu kuirejesha kwa wakati ili iweze kuwanufaisha Wananchi wengine.
Naye Mkurugenzi wa Wakala wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhan Mohamed amesema lengo la taasisi hiyo ni kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuwapatia elimu ya masoko na kuwawekea mazingira mazuri katika uzalishaji na uuzaji wa bidhaa zao.
Amesema ZEEA imekuwa ikitoa mikopo kwa wajasiriamali ndani ya Zanzibar ikiwa ni moja ya jukumu lake la msingi ambapo hadi kufikia mwezi wa Agost 2023 imetoa jumla ya Bilioni 20.2 kwa wajasiriamali na wafanyabiashara mbali mbali nchini.
Naye Ubwa Omar ambaye ni mnufaika wa na mikopo inayotolewa na ZEEA amewataka wananchi kuzitumia fursa za mafunzo na mikopo zinazotolewa ili kujikwamua kichumi ambapo mkopo huo umemsaidia kuendesha taasisi yake ya Iland Diary na kuajiri Vijana Saba kupitia taasisi hiyo.
Tamasha hilo ni la kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwaTaasisi ya Wakala wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar imeanzishwa mwezi March 2022 ambapo kauli mbiu ni “Tuwawezeshe wananchi, tutengeze ajira kwa kuimarisha uchumi endelevu Zanzibar”