Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Dkt. Selemami Jafo akishuhudia wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakipanda mti katika viwanja vya Bombambili mjini Geita ambako maonesho ya Teknolojia ya Madini yanaendelea, Waziri Dkt Selemami Jafo ameshiriki katika zoezi la upandaji wa miti hiyo.
………………………….
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itaendelea kusimamia sera na miongozo pamoja na kutoa maelekezo kwa taasisi za fedha wanazozisimamia ikiwemo mabenki ili kuhakikisha wanafanya shughuli zao pamoja na kutunza mazingira jambo ambalo litasaidia kufikia malengo katika maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza leo Septemba 25, 2023 na Waandishi wa Habari kuhusu siku ya upandaji miti na utunzaji wa mazingira katika Maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea kwenye Viwanja vya Bomba mbili – EPZ Mkoani Geita, Kaimu Meneja kitengo cha Mawasiliano BoT, Noves Mosses, amesema kuwa wanaendelea kutoa maelekezo kwa taasisi za fedha jinsi ya kufanya kazi zao na kutunza mazingira.
Amesema kuwa taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo Benki ya CRDB kupitia “Kijani Bond” wameanza kutekeleza maelekezo ya BoT katika kuhakikisha wanatunza mazingira.
“Kijani Bond inaenda kutoa maelekezo kwa watanzania na wadau mbalimbali ili watunze mazingira na kuwa endelevu” amesema
Amesema kuwa programu zote zinazotekelezwa na taasisi za fedha lazima zipate baraka kutoka benki Kuu, huku akibainisha kuwa kila Kiwanda kinachoanzishwa kinahakikisha hakuna uharibifu wowote wa vyanzo vya maji pamoja na misitu.
Ameeleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania ni mdau wa mazingira hivyo watahakikisha taasisi zote za fedha ambazo zipo chini yao wanafanya shughuli zao zinafanya kazi ya kutunza mazingira kwa namna moja au nyengine.
“BoT leo tumeshiriki zoezi la upandaji wa miti, tutaendelea na zoezi hili kama sera yetu inavyotuelekeza kushirikiana na jamii katika kufanya miradi mbalimbali ambayo inakwenda kuboresha mazingira” amesema
Amefafanua kuwa wanatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo upandaji wa miti, kusafisha mazingira katika maeneo mbalimbali ikiwemo fukwe ikiwa ni utekelezaji wa sera ya kuisaidia jamii katika utuzaji wa mazingira.
Amesema kuwa BoT ina wajibu wa kuweka mazingira vizuri katika maisha ili kuepuka changamoto ambazo zinaweza kujitokeza.
“Uchumi wetu unakuwa endelevu kwa kujali mazingira katika sekta tofauti ikiwemo wachimbaji wa madini, wakulima ili tupige hatua katika maendeleo” amesema
Ametoa wito kwa jamii na wadau mbalimbali kutunza mazingira ikiwemo vyanzo vya maji, miti ili kulinda uchumi wa Tanzania uwe na tija.