Mkurugenzi wa Kituo cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini profesa Juvenal Nkonoki akitoa cheti cha ushiriki wa mafunzo
Washiriki wakiendelea na mafunzo.
Mrajisi msaidizi Mkoa wa Pwani Abdilah Abasi akizungumza na washiriki wa mafunzo.
Washiriki wa mafunzo wakiwa ukumbini.
……..
Na Hellen Mtereko, Pwani
Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Juvenal Nkonoki amevitaka vikundi vya Wavuvi na Wachakataji dagaa vya Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kutumia maarifa ya ushirika waliyoyapata kujijenga kiuchumi.
Wito huo ulitolewa Ijumaa Septemba 22, 2023 katika hafla ya ufungaji wa mafunzo yaliyo fanyika kwa siku mbili ya kuwajengea uwezo wawakilishi wa vyama vya ushirika na vikundi 10 vya Wavuvi na Wachakata dagaa vyenye jumla ya Wanachama 1058 kati yao Wanawake 185 na Wanaume 873.
Mafunzo hayo ya misingi ya ushirika kwa vyama vya ushirika na vikundi yamefanyika katika Mji wa Bagamoyo Mkoani Pwani.
“Ndugu washiriki ninawaomba mkatumie mbinu za uongozi mlizozipata kuviwezesha vikundi na vyama vyenu vya ushirika kupata uchumi imara kwa mstakabali wa ushirika na mtu mmoja mmoja”. Alisema Prof. Nkonoki.
Profesa Nkonoki ameendelea kuishukuru Serikali ya Japani pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ufadhili wa mafunzo hayo pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uratibu wa mafunzo hayo yaliyo fanyika katika Wilaya za Mafia, Pangani na Bagamoyo.
Wakati huo huo mwakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Owen Kibona.amevitaka vikundi hivyo kutunza na kuzilinda rasilimali za uvuvi kwa kutumia njia sahihi ambayo Wizara inapendekeza.
Nae Mrajisi Msaidi wa Mkoa wa Pwani Bw. Abdilah Abasi amewapongeza Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Chuo cha Mipango kwa uratibu wa mafunzo hayo elekezi kwa vikundi na vyama vya ushirika vya wavuvi vya Mkoa wa Pwani.
Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Wavuvi na Wachakataji wa Dagaa ni moja kati ya malengo ya mradi wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu Nchini unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Chuo cha Mipango.