Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Doto Biteko akipata maelezo kutoka kwa Stella Marwa Meneja wa NIC Insurance Kanda ya Ziwa wakati alipotembelea katika banda la shirika hilo kwenye maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kwenye viwanja vya Bombambili mjini Geita Jumamosi Septemba 23,2023.
Stella Marwa Meneja wa NIC Insurance Kanda ya Ziwa akionesha moja ya bidhaa za bima zinazowasaidia wafanyakazi wa migodini katika banda la shirika hilo kwenye maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kwenye viwanja vya Bombambili mjini Geita Jumamosi Septemba 23,2023.
Wafanyakazi wa shirika la NIC Insurance wakiwa katika picha ya pamoja katika banda lao.
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM.
Shirika la Bima (NIC) limewataka wamiliki wa migodi nchini kukata bima za mashine za uchimbaji wa madini jambo ambalo litawasaidia kutekeleza majukumu kwa ufanisi na kuleta tija pamoja na kukabiliana na majanga yanayoweza kujitokeza.
Akizungumza leo Septemba 24, 2023 katika maonesho ya madini yanayofanyika katika Viwanja vya Bombambili mjini Geita, Meneja wa NIC Kanda ya Ziwa Bi. Stella Marwa, amesema kuwa wakati umefika kwa wachimbaji wa madini na wamiliki migodi kuchangamkia fursa ya kukata bima ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya uchimbaji wa madini.
Bi. Marwa amesema kuwa kuna bima ya Rehabilitation Bond ambayo inatoa uhakika wa kurejesha mazingira yaliyoharibika kutokana na shughuli ya uchimbaji wa madini na kurudi katika mazingira ya awali.
Amesema kuwa NIC pia inatoa bima ya Public Liability ambayo inawasaidia wachimbaji wa madini na wamiliki wa migodi kwa kuwalipa fidia wananchi waliopata madhara kutokana shughuli za uchimbaji wa madini.
“Endapo kuna madhara ya kemikali yamejitokeza kwa wananchi NIC itawasaidia kupunguza migogoro kati ya Serikali, wachimbaji wadogo na wamiliki wa migodi” amesema Bi. Marwa.
Aidha Bi. Stella ameeleza kuwa wanaendelea kutekeleza kwa vitendo agizo la Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dotto Biteko katika kuhakikisha wanatoa elimu ya bima ili kuwainua kiuchumi wachimbaji wadogo.